Membe: Kitakuwa kikao muhimu kwangu

Muktasari:

Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, Bernard Membe amesema kikao kitakachomuhoji kuhusu tuhuma za kimaadili zinazomkabili kitakuwa muhimu kwake akitumia neno, “nilikuwa nakisubiri sana.”

Dar es Salaam. Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, Bernard Membe amesema kikao kitakachomuhoji kuhusu tuhuma za kimaadili zinazomkabili kitakuwa muhimu kwake akitumia neno, “nilikuwa nakisubiri sana.”

Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM iliyoketi Desemba 13, 2019 iliagiza makada watatu wa chama hicho waitwe na kuhojiwa na Kamati ya Maadili na Usalama ya chama hicho baada ya kutuhumiwa kwa makosa ya kwenda kinyume na taratibu za chama.

Membe atahojiwa kesho Alhamisi Februari 6, 2020 mjini Dodoma.

Akizungumza katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Azam, Membe amesema ana amini kikao hicho kitakuwa kigumu huku akitumia neno ‘itategemea’, akimaanisha uamuzi utakaotolewa na kamati hiyo baada ya kumhoji.

Jana, ikiwa ni siku 52 zimepita tangu CCM kutangaza kuwaita wanachama wake watatu kuhojiwa,  Membe aliandika katika ukurasa wake wa Twitter, “hatimaye, jana (juzi) jioni nimepokea barua ya kuitwa kwenye kikao cha kamati ndogo ya udhibiti na nidhamu jijini Dodoma.”

Katika akaunti ya Twitter, ambayo mara kadhaa imekuwa ikitoa taarifa kuhusu mwanadiplomasia huyo, kuliandikwa: “Kikao kitafanyika Februari 6 2020 (kesho), saa 3 asubuhi kwenye jengo la White House. Nitahudhuria bila kukosa na bila kuchelewa! Stay  tuned!”

Wengine ambao wanapaswa kuhojiwa na kamati ya maadili ya CCM ni makatibu wakuu wa zamani wa chama hicho tawala nchini Tanzania, Abdulrahman Kinana na Yussuf Makamba

Alipoulizwa na mtangazaji aliyekuwa akimhoji kama atakuwa tayari kwa uamuzi wowote, Membe alijibu kwa ufupi, “Itategemea.”

Kuhusu jopo litakalomfanyia mahojiano, amesema kikao hicho kitaongozwa na makamu mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula, akidai mahojiano kuwa mazuri, yenye uwazi huku akitamani ushiriki wa wanahabari katika mahojiano hayo.

 “Ninawaambia watanzania, kesho ni siku muhimu sana, nilikuwa ninaisubiri sana kukutana na hii kamati na ninamuomba Mungu anijaalie niwepo katika kamati kwa sababu nitapata nafasi ya kuzungumza na wanakamati mambo wasiyoyajua na wanayoyajua.”

“Kwa hiyo kesho saa tatu asubuhi nisikosekane kwenda , niko sasa safarini kwenda Dodoma ili kesho tukazungumze. Kamati itasikiliza hoja na watatoa mapendekezo kwa halmashauri kuu ya Taifa ambayo itaamua kutoa uamuzi wowote, nadhani uamuzi utatoka mwishoni mwa mwezi huu Februari au Machi,” amesema Membe.

Baada ya mahojiano hayo, Membe amesema atakuwa tayari kuzungumza na wanahabari kwa kuwa suala hilo limekuwa wazi kwa umma tangu mwanzo.

Membe, Kinana na Makamba waliibua mjadala baada ya sauti zao kusikika mitandaoni wakizungumzia mpasuko ndani ya CCM, wameitwa sasa kuhojiwa kujibu tuhuma za kuvunja maadili.

Wakati vigogo hao wakitakiwa kuhojiwa, Halmashauri Kuu ya CCM iliwasamehe na kuwaonya wabunge wake watatu, January Makamba (Bumbuli), William Ngeleja (Sengerema) na Nape Nnauye (Mtama) ambao kwa nyakati tofauti walimuomba msamaha Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli.

Kinana na Makamba walikuwa wamewasilisha malalamiko yao CCM, Julai 14 2019 wakidai uongozi hauwalindi dhidi ya mtu ambaye amekuwa akiwadhalilisha na ambaye walimuelezea kuwa analindwa na mtu mwenye mamlaka.

Sauti hizo zilizoanza kusambaa mitandaoni baada ya waraka huo wa Makamba na Kinana walioupeleka kwa Katibu wa Baraza la Ushauri wa Viongozi wa CCM, Pius Msekwa kuwa umesambazwa kwenye vyombo vya habari.

Makamba na Kinana waliokuwa watendaji wakuu wa chama hicho tawala katika awamu ya nne, walitumia katiba ya CCM, toleo la 2017 ibara ya 122 kuwasilisha malalamiko yao ambayo yalizua mjadala ndani na nje ya chama hicho.

Membe anayedaiwa kutokuwa na uhusiano mzuri na viongozi wa juu wa CCM, itakuwa mara ya pili kufika mbele ya kamati hiyo.

Mara ya kwanza ilikuwa Februari 10, 2014 akiwa na wenzake Ngeleja (aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini) na Makamba (akiwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia).

Wengine walioitwa ni Edward Lowassa na Frederick Sumaye waliowahi kuwa mawaziri wakuu na Steven Wasira, aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais.

Adhabu

Kanuni za uongozi na maadili za CCM toleo la 2017 zimebainisha adhabu tatu kwa wanachama wanaofika mbele ya kamati hiyo.

 Katika kanuni hizo kifungu cha 5(2) kinasema; wanachama wanaovunja maadili ya chama kama yalivyoainishwa katika katiba ya CCM na kanuni za CCM wanachukuliwa hatua za kuwarekebisha na kama itashindikana kuwarekebisha ni kuwaondoa katika chama au katika uongozi.