Membe ajitokeza akiacha maswali

Mgombea Urais wa chama cha ACT Wazalendo,Benald Membe akizungumza na Wahariri wa vyombo vya habari nchini kuhusu michakato ya Uchaguzi  mkuu unaotarajia kufanyika 28 mwezi huu. Kushoto ni Mgombea mweza Prof Omari Faki Picha na Said Khamis

Muktasari:

Unaweza kusema mgombea urais kupitia ACT-Wazalendo, Bernard Membe ameacha maswali kutokana na majibu yake kuhusu kusuasua kufanya kampeni na viongozi wa chama chake kumuunga mkono mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu.

Dar es Salaam. Unaweza kusema mgombea urais kupitia ACT-Wazalendo, Bernard Membe ameacha maswali kutokana na majibu yake kuhusu kusuasua kufanya kampeni na viongozi wa chama chake kumuunga mkono mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu.

Kwa nyakati tofauti, kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye anawania urais Zanzibar wamenukuliwa kumuunga mkono Lissu.

Baada ya ukimya wa siku kadhaa za kutofanya mikutano ya kampeni, jana katika mkutano wake na wanahabari, Membe alisema yeye ndiye mgombea urais wa chama hicho na kwamba tayari ameshapeleka marekebisho ya ratiba yake ya kampeni kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), akisema ikitoka ataendelea na kampeni.

Hata hivyo, Zitto alipoulizwa na Mwananchi alisema msimamo wa chama hicho ni kumchagua Lissu.

“Nitampigia kura Lissu na wana ACT Wazalendo watampigia kura Tundu Lissu. Hakuna muda wa kuzunguka zunguka. Watanzania wanataka mabadiliko.”

“Sisi ndio viongozi wa ACT Wazalendo maelekezo yetu kwa Wanachama ni hayo, kuwa apigiwe kura Tundu Lissu,” alisema Zitto kupitia mtandao wa Whatsapp akijibu swali la Mwananchi.

Aahidi kufanya kampeni za lala salama

Tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi Agosti 26, mwaka huu, Membe amefanya mikutano mitatu pekee katika mikoa ya Pwani na Lindi, kisha kusafiri nje ya nchi na aliporejea akiwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) msaidizi wake alikamatwa, sababu aliyoieleza jana kuwa ndio ilimfanya ashindwe kuendelea na kampeni.

“Nawaeleza kwamba mimi Membe ni mgombea halisi wa ACT Wazalendo chama chetu kizuri na tutakipeleka mbele kuelekea Oktoba 28.

“Nitakuwa full swing (nitajitosa kikamilifu) katika dakika za lala za salama nikitoka benchi, kwa sababu nataka kufunga bao dakika za 89. Tumefanya kazi kubwa huku chini. Mtashuhudia tunafunga dakika ya 89,” alisema Membe.

Suala la Membe kutofautiana na viongozi wa chama hicho limezua maswali, lakini Membe alipoulizwa, alisema hakuna mgogoro ndani ya chama hicho

“Sisi tuko wamoja na hatuna mgawanyiko wowote, waliosema ni individuals (watu binafsi) na tumeyamaliza,’’ alisisitza.

“Wapo watu ndani ya CCM hawatampigia kura Magufuli, wapo watu ndani ya Chadema hawatampigia kura Lissu kabisa, wapo watu ndani ya ACT hawatampigia kura Membe,” alisema Membe.

Alipoulizwa kuhusu Zitto na Maalim Seif ambao hawatompigia kura badala yake watampigia Lissu, alijibu:

“Wawili wameshasema lakini wanaweza kubadilisha gia angani, maana kura ni siri.” Aliwataka wanachama wa ACT Wazalendo na Watanzania wote kuwaunga mkono wagombea wa chama hicho, huku akisema chama hicho kitashinda kikiwa peke yake.

“Katika siku nane zilizobaki naomba Watanzania wote walionipigia simu mkisema Membe usipogombea kura hatutapiga kura, nawaambia twendeni sasa,’’alisema.