Membe atangaza kuibuka dakika za lala salama

Muktasari:

Bernard Membe, mgombea urais kupitia ACT-Wazalendo amesema bado ni mgombea wa chama hicho licha ya kuelezwa kuwa yupo kimya, kubainisha kuwa sasa ataibuka dakika za lala salama, akijifananisha na mchezaji aliyeingizwa uwanjani dakika za 89.

Dar es Salaam. Mgombea urais kupitia ACT-Wazalendo, Bernard Membe leo Jumatatu Oktoba 19, 2020 amesisitiza kuwa bado ni mgombea wa chama hicho na ataibuka dakika za lala salama kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020.

Tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi Agosti 26, 2020, Membe amefanya mikutano mitatu katika mikoa ya Pwani na Lindi na baadaye hapo akasafiri kwenda Dubai kuhudhuria mkutano na uchunguzi wa afya yake, tangu aliporejea Tanzania amekuwa kimya.

Kauli ya Membe imekuja wakati Ijumaa Oktoba 16, 2020 viongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe alitangaza kumpigia kura mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni mjini Kigoma.

Mbali na Zitto, Mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad aliwahi kutangaza kuwa chama hicho kitamuunga mkono Lissu katika urais. Lissu pia aliwahi kutangaza kuwa Chadema itamuunga mkono Maalim Seif katika urais wa Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Membe amesema kukaa kwake kimya hakumaanishi kuwa hagombei.

"Wengi wameuliza Membe yuko wapi? Au amesimama? Au ameunga mkono juhudi? Nawaeleza kwamba mimi Bernard Camilus Membe ni mgombea halisi wa ACT Wazalendo chama chetu kizuri na tutakipeleka mbele kuelekea Oktoba 28.”

"Nitakuwa full swim katika dakika za lala za lala salama kutoka benchi kwa sababu nataka kufunga bao dakika za 90. Tumefanya kazi kubwa huku chini. Mtashuhudia tunafunga bado dakika 89. Watanzania," amesema Membe.

Huku akimtambulisha  mgombea mwenza Profesa Omar Fakhi, Membe amesema muungano wa vyama vya upinzani hauwezi kuiondoa CCM madarakani.

"Ipo nadharia inayosema vyama vikiungana vinatengeneza nguvu ya kuitoa CCM. Ukiangalia juu juu unakubali kwamba umoja ni nguvu utengano ni udhaifu. Tangu nchi za Afrika zipate huru nadharia hii haitekelezeki," amesema Membe.

 Aliendelea kutoa mifano ya madikteta waliowahi kutawala Afrika akisema hawakuwahi kuondolewa kwa muungano wa vyama.

 "Nadharia hiyo haijawa tested Afrika ika prove (ikaleta majibu) kweli bara lote la Africa," amesema.

Pia amesema kati ya vyama vya ukombozi 19 vya Afrika, vyama 13 havikuondolewa na muungano wa wapinzani.

"Vilivyoondolewa havikuondolewa na coalition bali vyama vimejitafuna vyenyewe. Ndipo vyama vikachukua hiyo advantage. Ili chama tawala kiondoke, lazima kuwe na mpasuko ndipo.”

"Mazingira hayo ya kupasuka kuwezesha wapinzani kushinda, yamekomaa Tanzania, yameiva na yamekomaa. Yale nitakayosema chama tawala tunakiangusha mwaka huu," amesema.

Akifafanua zaidi, Membe amesema ni dalili ya watu kuchoka, “angalieni kilichotokea baada ya kura ya maoni CCM wengi walienguliwa.”