VIDEO: Membe azungumzia tume huru ya uchaguzi 2020

Dar es Salaam. Aliyekuwa kada wa Chama Cha Mapinduzi CCM, Bernard Membe amesema anaunga mkono wanaodai kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi kabla ya Oktoba 2020.


Membe ametoa kauli hiyo akiwa nje ya CCM akisubiri hatima ya uanachama wake kutolewa na Halmashuri Kuu ya Taifa (Nec) ya chama hicho, baada ya kutimuliwa na Kamati Kuu (CC) Februari 28, 2020.


Juzi usiku wa saa 5:00 waziri huyo wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kupitia akaunti yake ya Twitter aliandika kuwa miongoni mwa mambo aliyoyazungumza alipokuwa mbele ya Kamati ya Maadili ya CCM chini ya mwenyekiti wake, Philip Mangula ni umuhimu wa kuwa na tume huru ya uchaguzi.


“Nilisema hili katika Kamati ya Maadili na ngoja niliseme tena; hali ya kiasiasa inayoendelea inathibitisha umuhimu wa kuwa na tume ya uchaguzi ambayo ni huru, yenye uwakilishi na inayoendeshwa kwa uwazi katika ngazi ya Taifa na ile ya chini. Kwa maana hiyo naunga mkono kwa nguvu sauti zote zinazopazwa kuwezesha suala hilo,” alisema Membe.