Meneja kampuni inayojenga SGR ahukumiwa Kisutu

Meneja wa mradi wa ujenzi wa Reli ya kisasa kampuni ya  Yapı Merkezi Yetkin Gen Mehmen raia wa uturuki (kushoto) akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo baada kukamatwa akisafirsha pesa kiasi cha dola 84850 za kimarekani. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Mahakama imemuhukumu kulipa faini ya Sh100 milioni au kwenda jela miaka mitatu  huku ikitaifisha dola za Marekani 84, 850 alizoshindwa kuzitolea maelezo baada ya kukutwa nazo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA)

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu Meneja Uwezeshaji wa Kampuni ya Yapi Merkezi inayojenga reli ya kisasa (SGR), Yetkin Gen  Mehmen kulipa faini ya Sh100 milioni au  kwenda jela miaka mitatu  huku ikitaifisha dola za Marekani 84, 850 alizoshindwa kuzitolea maelezo baada ya kukutwa nazo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA)

Mehmen ambaye ni raia wa Uturuki amehukumiwa na mahakama hiyo  leo Alhamisi Februari, 27, 2020 baada ya kukiri  kosa la kushindwa kutoa tamko ama maelezo ya fedha alizokutwa nazo dola za Marekani 84,850 katika Uwanja wa Ndege wa JNIA.

Akitoa hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesema kutokana na mshtakiwa huyo kukiri kosa lake mahakama hiyo imemtia hatiani.

"Mahakama inakuhumu kulipa faini ya Sh100 milioni au kwenda jela miaka mitatu pia fedha ulizokutwa nazo ambazo dola za Kimarekani 84,850 zinataifishwa na kuwa mali ya Serikali ya Tanzania," amesema  Simba.

Awali Wakili wa Serikali Mkuu, Shadrack Kimaro alimsomea hati ya mashtaka  mshtakiwa huyo kuwa Februari 13, 2020 eneo la Uwanja wa Ndege wa JNIA, alikamatwa  akiwa na begi la mkononi ndani yake kukiwa na dola za Marekani 84,850.

Kimaro alidai baada ya mshtakiwa huyo kukamatwa na dola hizo maofisa wa polisi walipomuuliza alishindwa kuzitolea maelezo.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo bado hajalipa kiasi hicho cha fedha ili aweze kuachiwa huru.