Meya Ubungo autaja wimbo wa CCM mahakamani, adai unawakandamiza wapinzani

Muktasari:

  • Meya wa Ubungo, Boniface Jacob ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa wimbo unaotumiwa katika shughuli na mikutano ya CCM wenye maneno ‘wapinzani tuwalete tuwachane tuwatupe’, unawahamasisha wananchi kuwanyima kura wapinzani.

Dar es Salaam. Meya wa Ubungo, Boniface Jacob ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa wimbo unaotumiwa katika shughuli na mikutano ya CCM wenye maneno ‘wapinzani tuwalete tuwachane tuwatupe’, unawahamasisha wananchi kuwanyima kura wapinzani.

Jacob ambaye pia ni diwani wa Ubungo ametoa kauli hiyo leo Jumatano Januari 22, 2020 wakati akitoa ushahidi katika kesi hiyo ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema mbele ya hakimu mkazi mkuu, Thomas Simba.

Meya huyo ambaye ni shahidi wa 10 katika kesi hiyo alieleza hayo baada ya kuulizwa na wakili wa upande wa utetezi, Peter Kibatala anaelewa nini kuhusu maneno yanayotumiwa wakati wa uchaguzi ya kuchinja na kichinjio (kitambulisho cha mpigakura).

Viongozi hao wa Chadema wanakabiliwa na mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi wanayodaiwa kuyatenda Februari 16, 2018 katika viwanja vya Buibui, Mwananyamala katika mkutano wa kufunga kampeni za ubunge wa Kinondoni.

“Kuna  kawimbo  umekasikia kana maneno wapinzani tuwachukue tuwachane tuwatupe,  kwa uelewa wako maneno hayo yana maana gani,” amehoji Kibatala.

Akiongozwa  na Kibatala, meya huyo amesema kichinjio kama ilivyoainishwa kwenye mashtaka ni kitambulisho cha kupiga kura kinachotumika katika chaguzi mbalimbali na kwamba kuchinja ni kunyima kura.

"Harambee, harambee, harambee, wapinzani tuwalete, tuwachane tuwatupe, CCM tuwalete tuwakumbatie tuwabusu,” amesema Jacob akirejea kutaja maneno yaliyo katika wimbo huo ulioimbwa na Kapteni John Komba (marehemu).

Awali, wakili wa Serikali mkuu, Faraja Nchimbi alipinga swali kuhusu wimbo huo lakini Hakimu aliruhusu swali kuulizwa na shahidi huyo akaeleza kuwa wimbo huo unalenga kuwanyima kura wapinzani.

Kuhusu mashtaka yanayowakabili viongozi  hao wa Chadema, Jacob alitaja viongozi waliojitokeza na kuzungumza katika mkutano huo akiwemo mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa aliyedai alihamasisha wananchi kufanya mabadiliko, John Heche (Tarime Vijijini) aliyehamasisha vijana kuwa na mwamko wa kupiga kura siku ya uchaguzi.

Amedai baada ya mkutano huo kumalizika, viongozi wa Chadema waliondoka wakisindikizwa na maofisa wa polisi waliokuwa wameimarisha ulinzi tangu mwanzo wa mkutano huo.

Mbali na Heche na Mchungaji Msigwa, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe;  katibu mkuu, John Mnyika; naibu katibu mkuu- Zanzibar, Salum Mwalimu; Dk Vicent Mashinji; mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama,  kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji jinai.