Meya wa Iringa ang’olewa madarakani

Madiwani wa baraza la manispaa ya Iringa wakiwa katika ukumbi wa Manispaa wakisubiri mkutano maalum wa baraza la madiwani ambao unaajenda ya kumuondoa Meya Alex Kimbe madarakani.

Muktasari:

Leo Jumamosi Machi 28, 2020 Baraza maalumu la madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa nchini Tanzania limepiga kura ya kumwondoa madarakani meya wa manispaa hiyo, Alex Kimbe ambapo kura 14 kati ya 26 zimeridhia kumwondoa.

Iringa.  Wajumbe wa Baraza maalumu la madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa nchini Tanzania wamemuondoa madarakani meya wa manispaa hiyo, Alex Kimbe.

Kimbe ambaye anatokana na chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema ameng’olewa madarakani leo Jumamosi Machi 28, 2020 katika kikao maalum cha madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa hiyo.

Akitangaza matokeo ya kura zilizopigwa, mwenyekiti wa kikao ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa, Joseph Ryata amesema wajumbe waliohudhuria kikao ni 26 na kura 14 zimeridhia kumuondoa meya huyo.

“Ndugu zangu wajumbe, kura zilizopigwa ni 26, kura zilizoharibika ni 12, kura halali ni 14 na kura za ndio ni 14 na hapana ni kura zero (sifuri), hivyo Baraza la leo limepiga kura kihalali na taratibu zote zimezingatiwa,” alisema Ryata

“Kuanzia leo Machi 28, 2020 Alex Kimbe hatakuwa meya hadi taratibu zitakavyofuata na baada ya kusema hayo naomba mkurugenzi uahirishe kikao” amesema

Kabla ya kupiga kura mkurugenzi wa manispaa hiyo, Hamid Njovu alitoa utaratibu wa kupiga kura ya kumuondoa meya huyo.

Njovu alisema kura zinazopigwa ni za kumuondoa mustahiki meya madarakani baada ya tuhuma zake kuthibitishwa na tume ya uchunguzi.

“Kura zinapigwa kumuondoa mustahiki meya madarakani baada ya tuhuma zake kuthibitishwa na kamati ya uchunguzi” alisema Njovu akitoa maelekezo kabla ya upigaji kura

Akiahirisha kikao hicho, Njovu amesema kama Kimbe hajaridhika na uamuzi huo, anaweza kukata rufaa kwa waziri wa Tamisemi.

Miongoni mwa tuhuma ambazo alikuwa anakabiliwa nazo Kimbe ni matumizi mabaya ya madaraka ikiwamo kufanya uamuzi bila kuzingatia kanuni za kudumu za Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.

Tuhuma nyingine ni matumizi mabaya ya rasilimali za halmashauri hiyo ikiwamo kutumia gari la halmashauri kwa matumizi yake binafsi.

Kimbe ameondolewa ikiwa ni miezi kama miwili imepita tangu Januari 9, 2020 Baraza la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kumng’oa Meya Isaya Mwita anayetokana na Chadema kwa tuhuma kama hizo za matumizi mabaya ya madaraka.