Meya wa Ubungo atangaza kutogombea tena udiwani

Dar es Salaam. Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob ametangaza kutogombea tena nafasi ya udiwani wa kata ya Ubungo katika uchaguzi ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2020 nchini Tanzania.
Boniface Jacob ametangaza uamuzi huo kupitia mtandao wake wa Twitter unaotumia jina la @MayorUbungo ambapo ameandika, “Nimetangaza kung'atuka ktk udiwani kata ya Ubungo muda wa madiwani utakapo isha, sitogombea tena udiwani uchaguzi ujao..! Miaka 10 utumishi wangu ni kwa sababu Wana-Ubungo mlinikopesha imani. Tumekuwa wote wakati wa shida na raha, mabonde na milima.”
Hatua hiyo inakuja siku kadhaa baada ya wanachama zaidi ya 2000 wa chama chake kutia saini na kumfuata nyumbani kwake kumtaka agombee ubunge wa jimbo la Ubungo katika uchaguzi mkuu ujao 2020.
Akizungumza na Mwananchi Digital, meya huyo amesema hatua yake ya kutogombea nafasi ya udiwani ni hatua ya pili baada ya ile ya wananchi kutaka agombee ubunge wa Ubungo na sasa anakiachia chama kama kitampa ridhaa atafanya hivyo.
“Wale wananchi niliwakubalia kwa moyo mmoja lakini mimi sio final, sina maamuzi kuna ngazi kama tatu za chama za kumpitisha mtu kugombea ubunge, najua wananipenda sana ila niliwaomba wasubiri maamuzi ya chama.”