Mfanyakazi TPA ahukumiwa kulipa fidia kwa kumuibia mteja gari la Sh400 milioni

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu aliyekuwa mfanyakazi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Omary Baya kulipa fidia ya Sh13.8 milioni baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu aliyekuwa mfanyakazi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Omary Baya kulipa fidia ya Sh13.8 milioni baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Baya na wenzake wanne ambao wao hawajakiri mashtaka yao wanadaiwa kuiba gari aina ya Toyota Land Cruiser VXR-V8 la Sh400 milioni mali ya kampuni ya Toyota Tanzania na kisha kuliuza kwa Sh83 milioni.

Baya ambaye alikuwa kitengo cha uchambuzi wa picha katika mamlaka hiyo,  ametiwa hatiani baada ya kukiri na kufikia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP).

Akisoma hukumu leo Jumanne Machi 31, 2020 Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega amesema mshtakiwa ametiwa hatiani kwa kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

"Mahakama imekutia hatiani kama ulivyoshtakiwa hiyo utatakiwa kulipa fidia ya Sh13.8milioni. Kiasi cha Sh3 milioni unatakiwa kulipa sasa hivi baada ya hukumu kutololewa na kiasi kilichobaki ambacho ni Sh10.8 milioni utakilipa ndani ya miezi sita kuanzia siku hukumu ilipotolewa,” amesema hakimu Mtega.

Mshtakiwa huyo alilipa Sh3 milioni kama sehemu ya malipo tangulizi walivyokubaliana na DPP.

Awali, wakili wa Serikali mwandamizi, Maternus Marandu na Ladslaus Komanya amedai shauri hilo liliitwa kwa ajili ya mshtakiwa huyo kusomewa maelezo ya awali baada ya kufanya majadiliano na DDP.

Akiwasomea maelezo yao, Komanya amedai mshtakiwa na wenzake wanne walijipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu kwa kuiba gari na kuliuza.

Mshtakiwa akiwa mwajiriwa wa TPA na wenzake April 11 na 12, 2019  walijipatia Sh83 milioni kutoka kwa Geofrey Kundi wakionyesha kuwa wao ndio wamiliki wa Toyota Land Cruiser VXR-V8 wakati wakijua ni uongo.

Komanya amedai kampuni ya Toyota Tanzania Limited April 2, 2019 iliagiza magari 32 aina ya Toyota Land Cruiser VXR-V8 kutoka Japan kupitia bandari ya Dar es Salaam.

Amedai baada kufika nchini utaratibu wa kuyatoa magari hayo bandarini ulianza na ndipo kampuni hiyo ilipobaini gari mmoja halipo na kutoa taarifa kwa mamlaka husika, uchunguzi ulifanywa na kubaini kuwa wafanyakazi wa TPA ndio waliohusika kuiba gari hilo.

Kabla ya kutolewa hukumu hiyo wakili wa utetezi, Singano Mhando aliiomba mahakama hiyo imuonee huruma mteja wake kwa kuwa hajaisumbua mahakama, pia ni mgonjwa wa kifua kikuu na amekaa ndani kwa zaidi ya miezi 10  na pia ana familia inayomtegemea.

Hata hivyo, hakimu Mtega alizingatia maombi hayo na kumhukumu kulipa fidia peke yake bila faini.