Mgogoro wa ardhi wasababisha maiti kurudishwa mochwari

Friday January 10 2020

By Anthony Mayunga, Mwananchi, [email protected] co.tz

Serengeti. Mwili wa Kitati Nyamsacha (80) mkazi wa eneo la Nyamatongo kitongoji cha Romakendo  kata ya Morotonga wilaya ya Serengeti mkoani Mara umelazimika kurudishwa chumba cha kuhifadhia maiti baada ya polisi kusitisha mazishi katika eneo hilo baada ya baraza la ardhi na nyumba kumpa ushindi mtu waliyekuwa wanashitakiana.

Nyamsacha alifariki Januari 6, 2020 nyumbani kwake kutokana na ugonjwa wa ini na kaburi lilichimbwa Januari 8,2020 na mwili wake ulitolewa chumba cha kuhifadhia maiti hospitali ya Nyerere siku hiyo kwa ajili ya mazishi yaliyokuwa yafanyike jana Alhamisi.

Walikutana na zuio la polisi kwa kutumia uamuzi ya baraza la ardhi na nyumba yaliyotolewa Oktoba 24, 2019 na mwenyekiti wake Kaare kutokana na maombi namba 65/2019 ya Beby Sambagita mkazi wa kijijini hapo.

Kamanda wa polisi wilaya ya Serengeti, Methew Mgema amewataka kutofanya kitu chochote katika eneo hilo  baada ya aliyepewa tuzo na baraza hilo kulalamika kuwa eneo lake limevamiwa na kuwataka watafute eneo lingine au wafuate taratibu za kisheria.

Mtoto wa mdogo wake na Nyamsacha, Mapambano Machaba leo Ijumaa Januari 9,2020 amesema wamelazimika kurudisha mwili chumba cha kuhifadhia maiti wakati wakiandaa taratibu nyingine za kisheria kwa kuwa hana eneo lingine la kumzika kwa kuwa toka mwaka 1994 alipouziwa na baba yake na aliyewazuia.

"Binafsi hatukujua kuna kesi yoyote maana alipofungua hapa marehemu baba yetu alishinda akakata rufaa Musoma ikaamriwa ianze upya hapa katani.”

Advertisement

“Hakuwahi kufungua tunashangaa kuona uamuzi mwingine ya kumpa haki kutoka kwa yule yule aliyeagiza isikilizwe upya na haikufanyika," amesema.

Kuhusu lini watafanya maziko, amesema kwa sasa hawezi kusema mpaka watakapomaliza vikao vya ukoo na kutoa uamuzi kama watazika au watachukua hatua za kisheria, ila kwa sasa kaburi wamelifunika kwa mabati wakisubiri muafaka wa familia.

Hata hivyo, Beby ambaye amepewa kisheria eneo hilo hakuweza kupatikana kijijini hapo huku taarifa zikidai kuwa anaishi Shinyanga na nyaraka hizo zilipelekwa na mtoto wake polisi.

Advertisement