VIDEO: Mgonjwa mwingine apona corona Tanzania

Dar es Salaam. Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema kuwa mgonjwa mwingine aliyekuwa na maambukizi ya virusi vya corona nchini amepona.


Waziri Ummy amesema hayo leo Ijumaa Aprili 03, 2020 katika taarifa aliyoitoa kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii ikiwemo akaunti ya Twitter ana Instagram.


Amesema kuwa mgonjwa mmoja aliyekuwa Ngara mkoani Kagera amepona na kufikisha idadi ya waliopona corona kuwa watatu.
“Mungu ni mwema. Na leo pia hatuna case mpya za COVID19. Mgonjwa wa Kagera (Ngara) amepona. Sasa jumla ya waliopona ni 3” ameandika waziri Ummy
“Mgonjwa aliebaki wa Arusha vipimo vyake siku ya 9 leo ni Negative. Tutampima siku ya 14 ili kujiridhisha kama amepona. Wagonjwa wengine 15 waliobaki wanaendelea vizuri,” amesema.


Waziri huyo ametoa rai kwa wananchi kuepuka misongamano na mikusanyiko na kufuata maelekezo ya wataalam ili kujikinga na maambukizi hayo
“Nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi kwa kuzingatia maelekezo ya wataalam wa Afya ili kujikinga na ugonjwa huu ikiwemo kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka. Sasa pia tuongeze nguvu katika kuepuka misongamano/mikusanyiko. Tuzingatie kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu,” amesema.