Mhasibu wa zamani TPA kizimbani

Wednesday January 15 2020

 

By Pamela Chilongola, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Aliyekuwa mhasibu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Stephano Mtui amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya zaidi ya Sh5.8 bilioni.

Akisoma hati ya mashtaka leo Jumatano Januari 15, 2020 mbele ya Hakimu Mkazi, Vicky Mwaikambo wakili wa Serikali, Faraji  Nguka amedai mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi.

Nguka amedai kati ya Julai 6, 2014 na Julai 8, 2014 katika bandari kavu ya Ami jijini Dar es Salaam,  mshtakiwa alighushi nyaraka  namba M144507872014  pamoja na risiti namba 432675 ya malipo ya zaidi ya Sh2.6 milioni ya bandari kutoka kwa kampuni ya Anchor Clearing and Fowarding

Amesema malipo hayo yalikuwa ya tozo ya bandari jambo ambalo halikuwa kweli.

Katika shtaka la tatu anadaiwa kati ya Julai, 2014 na Aprili 2015 katika eneo hilo mshtakiwa anadaiwa kuiba zaidi ya Sh5.8 bilioni.

Shtaka la nne la anadaiwa kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh5.8 bilioni.

Advertisement

Katika shtaka la tano anadaiwa kati ya Julai 2014 na Aprili 2015 mshtakiwa huyo akiwa na wenzake walifanya miamala ya Sh5.8 bilioni wakijua wazi kuwa ni zao la wizi.

Baada ya kusoma hati ya mashtaka, Nguka amedai upelelezi wa shauri hilo bado  haujakamilika, kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 20, 2020.

Advertisement