Migogoro ya ardhi, mfumo dume vyatajwa kuwa kero wananchi wa Korogwe, Lushoto

Monday August 19 2019

By Burhani Yakub, Mwananchi [email protected]

Lushoto. Mawakili kutoka mikoa mbalimbali nchini Tanzania wamebaini migogoro ya ardhi na mfumo dume kuwa changamoto zinazowakabili zaidi wakazi wa Wilaya za Lushoto na Korogwe mkoani Tanga.

Wamebaini hayo katika siku mbili za kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi hao na kuzinduliwa na mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kissa Gwakisa.

Mawakili hao ni kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto  walioshirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Mlezi wa chuo hicho, Iddy Mshana amesema katika siku mbili hizo mawakili na mahakimu walitoa msaada huo wa kisheria bila malipo kwa wakazi wa  Bumbuli, Mlalo na Lushoto na kubaini wengi wanakabiliwa na matatizo ya ardhi na mfumo dume.

“Kati ya wananchi 350 waliojitokeza kwenye vituo tulivyoviweka Bumbuli, Mlalo na Lushoto, 310 wanakabiliwa na migogoro ya ardhi wakati Mombo walijitokeza wananchi 97 huku wanawake 76 wakilalamikia kubaguliwa katika umiliki wa ardhi  na kutoshirikishwa kwenye maamuzi,” amesema Mshana.

Mwenyekiti wa TLS mkoani Tanga, Tumaini Bakari amesema baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi, mawakili waliwaeleza hatua za kufuata katika vyombo vya sheria ili kupata haki zao.

Advertisement

Kwa upande wake Gwakisa aliwataka mawakili kutumia taaluma yao kuwasaidia wananchi ambao baadhi yao wanafungwa au kunyang’anywa haki zao kutokana na kutokuwa na ufahamu wa kisheria.

Katibu tarafa ya Lushoto, Herieth Suta amesema asilimia 90 ya migogoro anayoipokea inahusu ardhi na kwamba inatokana na jiografia ya eneo hilo ikilinganishwa na idadi kubwa ya watu.

 


Advertisement