Mikiki ya uchaguzi wa KKKT ilivyomrudisha Dk Shoo katika uongozi

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limemrejesha madarakani, Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dk Frederick Shoo kuliongoza kanisa hilo.

Haikuwa kazi rahisi, Dk Shoo kurejea madarakani, hasa kutokana na kampeni za kutaka mabadiliko kutawala uchaguzi huo.

Hata hivyo, wajumbe 144 kati ya 218 hatimae walimpigia kura ya kuendelea kumhitaji Askofu Shoo aendelee kuliongoza kanisa hilo kwa kipindi kingine cha miaka minne.

Uchaguzi huo, ambao ulitanguliwa na mkutano wa 20 wa kanisa hilo, ulifanyika katika chuo kikuu kishiriki cha Tumaini- Makumira, ulianza Agosti 20, mwaka huu.

Hoja ya wachungaji wanawake

Licha ya ajenda kadhaa kujadiliwa na wajumbe wa mkutano huo, lakini hoja kuu ilikuwa ni uchaguzi na nafasi ya wanawake kuendelea kuteuliwa kama wachungaji katika dayosisi za kanisa hilo.

Wajumbe hao, pia walizungumzia suala la uenezaji wa huduma za kiinjili na taarifa za utendaji katika kanisa hilo kubwa nchini, lenye jumla ya Dayosisi 26.

Katibu mkuu wa KKKT, Brighton Kilewa, Askofu Shoo aliyekuwa anamaliza awamu yake ya kwanza kuliongoza kanisa na maaskofu wengine, walifanya kazi kubwa kufafanua hoja mbalimbali za wajumbe.

Kutokana na historia ya kanisa hilo lililoingia nchini tangu mwaka 1938, hoja ya wanawake kuwa wachungaji ilizua mjadala mkubwa hasa katika dayosisi ya Mbulu na Shinyanga.

Waumini wa dayosisi hizi, walielezwa hadi sasa hawaungi mkono, mpango wa kuruhusu kuteuliwa wachungaji katika makanisa yao.

Wajumbe katika mkutano huo, walitoa hoja mbalimbali juu ya suala hilo, ikiwepo kuzingatia historia ya kanisa lakini pia uamuzi wa mkutano mkuu uliofanyika Dodoma juu ya nafasi ya wanawake katika kanisa hilo.

Mjumbe wa mkutano huo, Magdalena Mathayo ambaye ni muithilogia kutoka Dayosisi ya Mbulu kitengo cha wanawake, anasema wanaopinga hoja hiyo ni waumini wachache ambao wanapaswa kuelimishwa.

Magdalena alisema wanawake sasa wamesoma na wanauwezo wa kuendesha ibada, ila kuna baadhi ya waumini wanapinga bila sababu wakijikita katika historia.

“Pale Mbulu kwa sasa tupo wanawake wanne ambao tumesoma na tuna uwezo wa kuwa wachungaji, lakini kuna vikundi vya waumini hawana imani na wanawake hili ni jambo la kuelimishwa tu,” alisema.

Mkurugenzi wa Idara ya wanawake na watoto Dayosisi ya Pare, Rosemary Solomon alisema jambo la wanawake kuwa wachungaji tayari lilipitishwa na kanisa hilo na ndio sababu katika baadhi ya dayosisi wanafanyakazi nzuri.

“Leo kuonekana bado kuna dayosisi hazitaki wanawake kuwa wachungaji, ni tatizo, nilitegemea leo kutolewa msimamo mmoja kuwa wanawake wanaweza kuwa wachungaji katika dayosisi zote,” alisema.

Hata hivyo, baada ya mjadala huo, Askofu Shoo alitoa maelekezo kwa maaskofu wa dayosisi nyingine na wajumbe wa halmashauri kuu kwenda kutoa elimu kwa baadhi ya waumini ambao hawalifahamu vyema jambo hilo.

Dk Shoo alieleza katika mkutano mkuu ujao jambo hilo inatarajiwa litakuwa limepata ufumbuzi.

Askofu Stevin Munga wa Dayososo ya Kaskazini Mashariki, alitaka waumini wa kanisa hilo kutobaguana kwani wote ni kitu kimoja, hakuna sababu ya kutengana.

Ulinzi mkali

Nje ya ukumbi ulinzi ulikuwa umeimarishwa na baadhi ya wajumbe kutoka Dayosisi za Kusini, Mashariki na Pwani na Kanda ya Ziwa, walikuwa na kampeni za kutaka mabadiliko.

Mmoja wa wachungaji kutoka kanda hizo, alieleza sababu za kutaka mabadiliko ni kurejesha mshakamano na taasisi mbalimbali, pia ukanda wa Kusini upate mkuu wa kanisa hilo.

Hata hivyo, wajumbe wengine hasa kutoka Dayosisi za mikoa ya Kaskazini, walikuwa na kampeni za kutaka Dk Shoo apewe fursa ya kumaliza muda wake wa vipindi viwili kama ilivyo desturi ya kanisa hilo.

Kikao cha maaskofu kwa mujibu wa Katiba ya kanisa hilo, ndicho hupitisha majina ya wagombea wa nafasi ya Mkuu wa Kanisa hilo na baadaye kuyapeleka katika halmashauri kuu na mkutano mkuu kwa ajili ya kupigiwa kura ili mshindi mmoja apatikane.

Kikao hicho ambacho kilikuwa kikisubiriwa kwa hamu, kilianza saa 10 jioni hadi saa tano usiku yalipotoka majina mawili, Askofu Shoo na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, Abednego Keshamshahara.

Saa 5:30 upigaji kura ulianza kwa majina mawili yaliyoanza kupigiwa kura, kwa utaratibu wa kura kupigwa kwa kufuata dayosisi moja baada ya nyingine.

Ushindi wa Dk Shoo

Baada ya mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi, Askofu Blaston Gavile wa Dayosisi ya Iringa, kutangaza matokeo kuwa, Askofu Shoo amepata kura 144 na Askofu Keshamshahara kura 74 kati ya kura 218, ukumbi uliripuka kwa shangwe.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Katiba ya KKKT, ilitakiwa mshindi kutangazwa baada ya kupata zaidi ya theluthi mbili za kura, lakini Askofu Keshamshahara alitangaza kujitoa ili uchaguzi kutorejewa.

Uamuzi wa Askofu Keshamshahara ulipokewa kwa shangwe na wajumbe wa mkutano huo, ambao walikuwa bado hawajatoka ukumbini.

Akizungumza baada ya kutangazwa, Dk Shoo aliwashukuru wajumbe wa halmashauri kuu, maaskofu na viongozi wote wa kanisa kwa kumchagua tena na kuwaomba kumuombea kwa Mungu atende vyema katika uongozi wake.

“Namshukuru Mungu, aliyependa nianze kazi hii tena…kunipa tena dhamana, namshukuru sana mdogo wangu Askofu, Keshamshahara, Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi, maaskofu na Rais wa fungamano la makanisa ya kilutheri,” alisema.

Askofu Dk Shoo, aliwaomba waumini wa KKKT na maaskofu wazidi kumuombea na kumpa ushirikiano.

“Mniombee na kunipa ushirikiano kama kanisa ili tutunze umoja wetu kama kanisa, sisi sote ni wafuasi wa bwana yetu Yesu Kristo,” alisema.

Askofu Masangwa, Bagonza watoa neno

Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Askofu Solomon Masangwa wa Dayosisi ya Kaskazini Kati, alisema anamshukuru Mungu kwa kuwapa kiongozi wa kanisa kwa kipindi kingine cha miaka minne. “naamini atasisimamia umoja wa kanisa, na kuimarisha mahusiano mazuri na Serikali ya awamu ya tano katika kuleta maendeleo na ustawi wa Watanzania wote bila kujali tofauti zetu”.

Askofu Benson Bagonza wa Dayosisi ya Karagwe, alisema kulikuwapo na hofu katika uchaguzi huo kuligawa kanisa, lakini hilo limeshindwa. “wanaotumiwa kujaribu kuligawa kanisa, wana uzoefu wa kuwagawa Watanzania kikanda, kiitikadi na kikabila ila wameshindwa”.

Alisema Kanisa lina itikadi zote, Kanda zote na makabila yote.

Waumini wazungumza

Mjumbe wa mkutano mkuu wa KKKT, Mary Lazer alisema, mkutano umekwisha kwa salama na kiongozi wa kanisa amepatikana, kazi kubwa wanayopaswa kuifanya sasa ni kuimarisha umoja baina yao na taasisi nyingine.

“Tumuunge mkono Askofu Mkuu, tuwe kitu kimoja katika kufanya kazi za kanisa letu,” alisema Laizer.

Kwa upande wake Emmanuel Saevie, alisema wajumbe wa mkutano mkuu, wamefanyakazi nzuri kumrejesha Askofu Shoo na sasa ni muhimu kusimamia vyema shughuli za kanisa.

“Napenda kumshauri mkuu wa kanisa aimarishe taasisi zetu kwa kutumia rasilimali watu iliyopo katika kusimamia kwa kiwango kinachotakiwa ili ziwe na manufaa kwa waumini na Watanzania kwa ujumla,” alisema.

Jonathan Kaaya, alisema misuguano ambayo ilijitokeza katika uchaguzi sasa inapaswa kuondolewa na viongozi wote kuwa kitu kimoja na kutoruhusu watu walio nje ya kanisa kuwaingilia na kuwagawa.

“Kama walikuwa na kambi zao za uchaguzi wavunje, turejee kuwa kitu kimoja kufanyakazi ya Mungu kwani kimsingi hakuna mtu ambaye ni mtimilifu kwa kila jambo,” alisema.

Mfanyabiashara Walter Maeda alitaka baada ya kukamilika uchaguzi, viongozi wote na waumini kurejea kufanyakazi za Mungu na kufuata taratibu na miongozo katika kanisa hilo.

Mkutano mkuu wa 20 wa kanisa hilo, umemchagua Askofu Dk Shoo, kuongoza kanisa hilo hadi mwaka 2023.

SOMA ZAIDI