Mirerani watii agizo la Serikali la mifuko ya plastiki

Saturday June 1 2019

By Joseph Lyimo, Mwananchi [email protected]

Mirerani. Wakazi wa Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wametii agizo la Serikali kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki ifikapo Juni mosi.

Wakizungumza leo Jumamosi Juni mosi 2019, baadhi ya wakazi hao wamedai kuwa hakuna namna ya kufanya zaidi ya kuzingatia agizo hilo la Serikali.

Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Haji Ngokwe amesema imemlazimu kuondoa mifuko yote ya plastiki iliyokuwa nyumbani kwake ili familia yake isipate matatizo.

"Nimefanya upekuzi kila mahali ili kuondoa mifuko yote iliyokuwa ndani ya nyumba yangu ili tusipate matatizo juu ya marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki inatupasa tugeukie vibebeo vingine mbadala," amesema Ngokwe.

Muuzaji wa samaki wabichi wa bwawa la Kidawash, Ally Ramadhan amesema wanapata wakati mgumu wa kubeba samaki wabichi kwani mifuko hiyo ya plastiki imepigwa marufuku.

Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Adam Kobelo amesema watu wengi wameitikia tamko la Serikali juu ya katazo la mifuko hiyo.

Advertisement

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Bryceson Kibassa amewataka wananchi kuhakikisha wameacha kutumia mifuko hiyo ili kutii agizo la Serikali.

Advertisement