VIDEO: Miss Tanzania kubebeshwa Kamusi za Kiswahili atakapokwenda Uingereza

Saturday August 24 2019

By Nasra Abdallah, Mwananchi

Dar es Salaam. Wakati shindano la kumsaka mrembo wa dunia mwaka 2019 likitarajiwa kufanyika Jijini Londoni nchini Uingereza, Serikali ya Tanzania imesema itampatia kamusi za Kiswahili mwakilishi wa Tanzania atakapokwenda kwenye mashindano hayo.

Hayo yamesemwa jana Ijumaa Agosti 23,2019 na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe katika fainali za kumsaka Miss Tanzania zilizofanyika jijini Dar es Salaam.

Waziri Mwakyembe alisema mrembo wa Tanzania hana budi kujivunia lugha hiyo kokote anakokwenda ikiwemo katika shindano hilo litakalokutanisha nchi mbalimbali duniani na kuongea kuwa Serikali itampatia kamusi za Kiswahili kwenda nazo.

 

"Ili kuhakikisha mrembo watu anakitangaza vizuri Kiswahili, tutampatia kamusi nyingi za lugha hiyo ili  akazigawe kwa warembo wenzake atakapokwenda nchi London kumsaka mrembo wa dunia ili nao waweze kujifunza lugha hiyo ambayo hivi karibuni imechaguliwa rasmi kuwa lugha ya nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc)," alisema Dk Mwakyembe.

Hata hivyo, waziri huyo alisema anasikitishwa  na kitendo cha  warembo wanaoshiriki shindano la Miss Tanzania kuendelea kutumia lugha ya Kingereza kujieleza pale inapofika hatua ya kuulizwa maswali wakati wana uwezo wa kuzungumza Kiswahili vizuri.

Advertisement

"Mtu umekazana kutumia Kingereza mwisho wa siku unajikuta unashindwa kujieleza vizuri na kuomba urudiwe kuulizwa swali kama baadhi tulivyowashuhudia kwenye shindano hilo.”

“Hii sio sahihi kwani aliyekuambia usipoongea Kingereza hautashinda nani, hebu warembo wetu wabadilike kupenda vya kwao," alisema Waziri Mwakyembe

Jaji Mkuu wa mashindano hayo, Shyrose Bhanji alisema hakuna mrembo anayelazimishwa kuzungumza Kingereza isipokuwa ni utashi wa muhusika kuamua atumie lugha ipi.

Advertisement