Miundombinu Dar es Salaam yatengewa bilioni 186

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Tawala za Mikoa na  Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jaffo akiwaslisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imeomba kuidhinishiwa na Bunge la Tanzania Sh 186.8bilioni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu.

Dodoma. Mradi wa Uendelezaji wa miundombinu katika jiji la Dar es Salaam umetengewa Sh186.8 bilioni katika mwaka wa fedha 2020/2021 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo leo Jumatano Aprili 7 2020, amesema fedha hizo ni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 47.9 kwa kiwango cha lami kwa mikataba na makandarasi inayoendelea.
Alitaja shughuli nyingine ni kuanza ujenzi wa barabara ya Nzasa-Kilungule-Buza (kilomita 7.6), Ulongoni-Bangulo-Kinyerezi (kilomita 7.5) na Magomeni Mapipa- Urafiki (kilomita 7.31) na barabara zenye urefu wa kilometa 11.7 kwa kiwango cha lami katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni.
Shughuli nyingine ni kuendelea na ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua yenye urefu wa kilometa 26, kukamilisha ujenzi wa masoko sita ya Kilakala, Kigilagila, Bomubom, Minazi Mirefu, Mbagala na Bwawani.
Nyingine ni Mpango wa Uendelezaji Ukanda wa Mabasi Yaendayo Haraka, kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani uliounganishwa na mfumo wa kijiografia wenye taarifa muhimu za vyanzo vya mapato.
Jafo ametaja shughuli nyingine ni ununuzi wa vifaa vya kufanyia usafi wa miundombinu ya barabara na mifereji ya maji ya mvua.