Mjadala Spika Ndugai kuzindua kamati za Bunge laivu Kenya

Spika wa Bunge, Job Ndugai (kush-oto) akiteta jambo na Spika wa Bunge la Kenya, Justin Muturi wakati wa hafla ya uzin-duzi wa kanuni za kudumu za Bunge la Kenya za lugha ya Kiswahili na taarifa za mwaka za utendaji kazi wa kamati uliofanyika juzi katika Bunge la Kenya jijini Nairobi. Picha na Ofisi ya Bunge

Mwanza/Dar. Tukio la Spika wa Bunge, Job Ndugai kuzindua vikao vya kamati za Bunge la Kenya ambavyo vitakuwa vikionyeshwa mubashara na vyombo vya habari limeibua hoja na maoni tofauti kutoka kwa wasomi, wanasiasa na wataalamu wa habari.

Walipoulizwa na Mwananchi kwa nyakati tofauti jana kutoa maoni yao kuhusu jambo hilo, baadhi ya wasomi, wanasiasa na wanahabari wamesema tukio hilo linapaswa kuwa funzo kwa Spika Ndugai mwenyewe, wabunge, Serikali na Watanzania kwa ujumla kuwa ‘Bunge laivu’ ni jambo muhimu.

“Kwa kuzindua vikao ‘laivu’ vya kamati za Bunge la Kenya ni ishara, ujumbe na uthibitisho kuwa Bunge laivu ni zuri na Spika Ndugai mwenyewe anapenda. Kwa mamlaka na nafasi yake ya uspika asaidie kurejesha bunge laivu,” alisema Deodatus Balile, kaimu mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Kauli inayofanana na hiyo ilitolewa na mwenyekiti mstaafu wa TEF, Absalom Kibanda aliyemwomba Spika Ndugai, viongozi na mamlaka za Serikali zilizosimamia na kutekeleza mchakato wa kuzuia Bunge kuonyeshwa moja kwa moja kwenye vyombo vya habari kutoona haya kujisahihisha.

“Viongozi wetu walifanya makosa kuzima Bunge laivu, nitashangaa kama hawajisikii vibaya na kujutia kosa hilo….hata Nape (Nnauye, aliyekuwa waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo) akiulizwa sasa hivi atakiri kuwa alifanya makosa. Tujisahihishe,” alisema Kibanda.

Kuhusu Spika Ndugai kushiriki kuzindua vikao vya kamati ya Bunge Kenya ambavyo vinaonyeshwa moja kwa moja, Kibanda alisema “simtetei Spika Ndugai….lakini naamini amejisikia vibaya na kufedheheka kwa kuzindua vikao laivu vya kamati za Bunge la Wakenya ambao vyomba vyao viliripoti sana tukio la kuzima Bunge laivu Tanzania.

Gharama na kauli zisizo na staha

Akizungumzia hoja ya kupunguza gharama kubwa ya kuonyesha Bunge laivu iliyotumiwa na Serikali kufikia uamuzi wa kuzima matangazo hayo ya moja kwa moja, Kibanda alisema hiyo ilikuwa ni kichaka tu cha kuzima kwa sababu vipo vituo binafsi vya runinga vilijitolea kuonyesha Bunge kwa gharama zao, lakini navyo vilizuiwa.

“Serikali na CCM ilihisi kuumizwa zaidi na Bunge laivu kutokana na michango ya wabunge wa upinzani walioonekana kujenga hoja zinazovutia umma. Jambo la msingi ingekuwa CCM kuwajengea uwezo wabunge na mawaziri kujenga hoja kujibu zile za upinzani,” alisema Kibanda.

Kuhusu kauli zisizo na staha na vurugu kutoka kwa wabunge wa upinzani, Kibanda alishauri “hoja sahihi ambayo ingekubalika na kuungwa mkono na umma ingekuwa kutumia kanuni kudhibiti lugha zisizo na staha na uvunjifu wa kanuni. Siyo kuzima Bunge laivu.”

Kujifunza kutoka Kenya

“Spika Ndugai achukulie tukio la yeye kuzindua vikao vya kamati za Bunge la Kenya ambavyo vitakuwa vinaonyeshwa moja kwa moja kama changamoto na funzo kuruhusu siyo tu vikao vya Bunge, bali hata vile vya kamati ambako ndiko hoja nyingi na za msingi hujadiliwa na kuamuliwa,” alisema Dk Onesmo Kyauke, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii.

Dk Kyauke ambaye pia ni wakili alisema Bunge ni chombo cha wananchi na wabunge hawawakilishi maoni au mawazo yao binafsi bali ya wapiga kura wao ambao wana haki ya kufahamu mijadala yote kuanzia vikao vya kamati hadi Bunge kwa ujumla.

Wanasiasa

“Nimeshangaa Ndugai kuzindua vikao laivu vya kamati ya Bunge la Kenya wakati yeye anapoongoza Bunge lisiloonyesha siyo tu vikao vya kamati, bali vikao vyote vya Bunge vimezimwa,” alisema John Mrema, mkurugenzi wa mawasiliano, itifaki na mambo ya nje wa Chadema.

Alisema waliomwalika na kumpa jukumu Spika Ndugai kuzindua suala hilo walipanga kumpa ujumbe na somo ambalo anaamini atalitumia vema akirejea nchini kwa kuruhusu Bunge laivu.

Kauli kama hiyo ilitolewa na mwenyekiti wa Chauma, Hashimu Rungwe aliyeenda mbali kwa kusema yawezekana Ndugai hakufahamu kama Wakenya wangempa kazi hiyo aliyosema haijamwachia taswira njema .

Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Suzan Lyimo alisema Spika Ndugai atakaporejea nchini anatakiwa kuwaeleza Watanzania juu ya mpango kama huo kutekelezwa hapa nchini ili kuongeza uwazi zaidi.

“Nadhani ni muda mwafaka kwa sisi pia kurejesha utaratibu wetu wa zamani wa kurusha vikao vya Bunge. Spika akija atueleze, kwa sababu ni jambo ambalo wananchi wengi wamekuwa wakililia siku zote,” alisema Lyimo.

Kwa upande wake, mbunge wa Kilwa, Seleman Bungara (Bwege) alisema Spika anatakiwa kujifunza kutoka kwa Wakenya na kuleta utaratibu huo hapa nchini ili kuimarisha demokrasia na uwazi.

Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa alisema Ndugai alikuwa mpambanaji wa demokrasia na haki nchini, lakini sasa amebadilika.

Dovutwa alisema kitendo cha Ndugai kuwapongeza Wakenya ni ishara kwamba anayajua mazuri yanayotakiwa kufanywa, lakini anashindwa kwa sababu ya kusukumwa na upepo badala ya utendaji.

“Nadhani siku hizi anasukumwa na upepo badala ya kusukumwa na utendaji,” alisema Dovutwa na kuongeza kuwa “tatizo lipo kwenye Katiba yetu, ile misingi ya kuwawajibisha viongozi haipo tena.”

Katibu mkuu wa CCK, Renatus Muabhi alisema Kenya ambayo ilikuwa nyuma ya Tanzania katika viwango vya demokrasia sasa ndiyo inaongoza na sasa wameenda mbele zaidi kwa kuongeza uwazi zaidi kupitia vikao vya kamati.