Mjerumani: Kauli ya Rais Magufuli imempa heshima Harmonize

Wednesday October 16 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Beauty Mmari maarufu  Mjerumani ambaye ni Meneja wa msanii Harmonize amesema kauli ya Rais wa Tanzania, John Magufuli imempa heshima na itaibua sifa na utendaji mwingine ulio ndani yake mbali ya muziki.

Rais Magufuli akiwa kwenye mwendelezo wa ziara ya siku nne mkoani Lindi alisema anatamani msanii Harmonize akagombee Ubunge Jimbo la Tandahimba.

 “Nampongeza sana Hamornize sijui anatoka jimbo gani? Tandahimba! Aah ningetamani kweli Hamornize aende kule akagombee akawe mbunge wa Tandahimba,” alisema Rais Magufuli

Akizungumzia kauli hiyo leo Jumatano Oktoba 16, 2019, Mjerumani amesema,“Kauli ya Rais inafikirisha, bila shaka ametafakari na kuona kabisa Harmonize anafaa kuitumikia jamii nje ya muziki.”

“Inafikirisha kwa sababu inawezekana hakuwa na mpango wa kufanya hivyo, lakini anaweza kufikiria kwa sababu imempendeza mkuu wa nchi na ameona anafaa, kwa kweli amempa heshima kubwa, ”amesema Mjerumani.

Mjerumani amefafanua kuwa, “Rais amepima, amemtathmini ndiyo maana akatoa kauli ile, itampa nguvu ya kufanya zaidi ya anachofanya sasa.”

Advertisement

“Akifanya hivyo atazalisha Harmonize mwingine alikuwa ndani yake lakini hakuwa anajulikana, ”amesema Mjerumani.

Katika mkutano aliohutubia Rais, Harmonize pia alitumbuiza.

Harmonize amekuwa akitumbuiza kwenye mikutano ya Rais na akiimba wimbo uitwao Magufuli ambao unaelezea miradi ya maendeleo aliyoifanya.

 

 

 

 


Advertisement