Mkandarasi atoweka eneo la mradi, Profesa Mbarawa aagiza aondolewe

Waziri wa Maji, Prof Makame Mbarawa akizungumza na wakazi wa kijiji cha Mbalibali wilayani Serengeti ambapo ameagiza Ruwasa kuvunja mkataba na mkandarasi aliyekuwa akitekeleza mradi wa maji kijijini hapo. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Waziri wa Maji nchini Tanzania, Profesa Makame Mbarawa ameagiza kuvunjwa mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji kijiji cha Mbalibali wilayani Serengeti baada ya mkandarasi kutoonekana eneo la kazi zaidi ya miezi 11.

Serengeti. Waziri wa Maji nchini Tanzania, Profesa Makame Mbarawa ameagiza kuvunjwa mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji kijiji cha Mbalibali wilayani Serengeti baada ya mkandarasi kutoonekana eneo la kazi zaidi ya miezi 11.

Ametoa agizo hilo leo Ijumaa Novemba 22, 2019 alipotembelea mradi huo kuangalia maendeleo yake. Utekelezaji wa mradi huo ulianza Juni, 2018 na ulitarajiwa kukamilika Juni, 2019.

Amesema mkataba wake utavunjwa na kuendeleza mradi ulipofikia.

“Ikifika Ijumaa ijayo nipate taarifa za kuvunjwa kwa mkataba ili niweze kuleta fedha na kazi ianze Jumatatu inayofuata. Hii kazi tutaifanya wenyewe maana huyu mkandarasi ni tapeli na wa ovyo ndio maana kaamua kukaa kimya bila kutoa taarifa yoyote,”amesema Mbarawa.

Amebainisha kazi hiyo itakayofanyika chini ya usimamizi wa wakala wa maji vijijini, itapaswa kukamilika ndani ya miezi miwili, kwamba fedha ipo kinachosubiriwa ni mkataba  kuvunjwa kisheria.

Kaimu meneja wa Wakala wa Maji Vijijini Wilaya ya Serengeti (Ruwasa), Andrew Kisaro amesema mradi huo unatarajiwa kuhudumia zaidi ya watu 7, 000 katika vijiji vya Mbalibali na Kitunguruma.

Amesema kuwa mkandarasi huyo hadi sasa ametekeleza mradi huo kwa asilimia 45 kulipwa Sh292 milioni. Amesema mradi wote unagharimu zaidi ya Sh1.1 bilioni.

Amebainisha kuwa baada ya mkandarasi huyo kuondoka eneo la kazi, ofisi yake imejitahidi kumtafuta bila mafanikio, “hatua tulizozichukua ni kumuandikia barua sita ambazo hakuzijibu.”

“Sasa tupo katika mchakato wa kuvunja mkataba na tayari wanasheria wa halmashauri wanashughulikia suala hilo, ndani ya wiki ijayo tutakuwa tumekamilisha mchakato huu.”