VIDEO: Mkapa akumbuka mauaji ya watu 21 Pemba, aeleza upungufu wake

Muktasari:

Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa amesema mauaji ya watu 21 kisiwani Pemba ni kati ya tukio lililotia doa katika uongozi wake wa miaka 10.

Dar es Salaam. Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa amesema mauaji ya watu 21 kisiwani Pemba ni kati ya tukio lililotia doa katika uongozi wake wa miaka 10.

Ametoa kauli hiyo leo Jumanne Novemba 12, 2019 katika uzinduzi wa kitabu chake cha Maisha Yangu, Kusudio Langu uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wastaafu na waliopo madarakani.

“Mauaji ya watu 21 Pemba, Zanzibar Januari mwaka 2001 nayakumbuka. Hili tukio litaendelea kuwa doa katika utawala wangu licha ya kuwa mimi sikuwepo,” amesema Mkapa aliyekuwa rais wa Tanzania mwaka 1995 hadi 2005.

Katika uzinduzi huo Mkapa pia alieleza upungufu wake kuwa ni kutokuwa rahisi kutoa pole.

“Upungufu wangu ilikuwa si rahisi kutoa pole lakini mrithi wangu Jakaya Kikwete ni mwepesi katika hili,” amesema Mkapa.

Mauaji hayo ya Januari 27, 2001 yalitokana na mgogoro wa kisiasa wakati polisi wakizima maandamano ya wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) waliokuwa wakipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2000.

Walikuwa wakipinga matokeo ambayo Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilimtangaza aliyekuwa mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Amani Abeid Karume kuwa Rais wa Zanzibar kwa kumshinda aliyekuwa mgombea wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad.

CUF walikuwa wanapinga matokeo hayo wakidai kwamba ‘yamepikwa’ na mgombea wao ndiye aliyekuwa ameshinda katika uchaguzi huo uliokuwa umeshirikisha vyama vingi vya siasa viwasini humo uliofanyika kwa mara ya pili tangu ule wa mwaka 1995.