Mkapa awashukia trafiki, rushwa

Monday November 18 2019

 

By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Unaweza kusema kwa kuwa Rais hupita na msafara wa magari ambao hausimamishwi na askari yeyote wa barabarani, hawezi kujua matatizo wanayokumbana nayo madereva wa magari ya kawaida.

Lakini si kwa Benjamin Mkapa, Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu. Pengine ni kwa kutumia vyombo vyake, Mkapa anajua vitendo vya askari wa usalama barabarani kudai rushwa kutoka kwa madereva.

Na hilo ameliweka katika kitabu chake cha “My Life, My Purpose (Maisha Yangu, Kusudi Langu)” kama moja ya mambo yanayomsikitisha, huku rushwa ikiwa moja ya ajenda zake muhimu wakati anaingia madarakani mwaka 1995.

Wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, CCM ilimnadi Mkapa kama mtu asiye na kashfa ya rushwa na akapewa jina la utani la Mr. Clean (Bwana Msafi) na ndiye aliyeunda Tume ya Jaji Joseph Warioba kubaini mianya ya rushwa.

Mkapa anasema hakuna kitu kilichokuwa kinamuumiza kama suala la rushwa na hasa kwenye taasisi za huduma.

“Nilikuwa naumia sana kusikia mtu mnyonge anaombwa rushwa ili aweze kupata huduma kama elimu, afya na haki nyingine,” anasema Mkapa.

Advertisement

Mkapa anasema ndio maana aliamua kuunda tume ya kuchunguza masuala ya rushwa chini ya Jaji Joseph Warioba ili kutoa mapendekezo mbalimbali ya namna ya kukabiliana na tatizo hilo.

Hata hivyo, anakiri hakuweza kumaliza tatizo hilo la rushwa wakati wa utawala wake na hadi leo linaendelea kuumiza wananchi.

Kero za trafiki

Mkapa amelalamikia kitendo askari wengi kujazana barabarani.

Rais huyo mstaafu amesema huwaona trafiki hao wakiwa wengi zaidi wakati zinapokaribia sikukuu na kudai kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kuwa ni kero kwa madereva.

Trafiki wanalalamikiwa kwa tabia ya kuchukua rushwa kutoka kwa madereva wa magari makubwa, madogo na waendesha pikipiki baada ya kubaini makosa dhidi yao.

Alisema ameambiwa askari hao huwabana madereva ili wapate fedha za kutumia wakati wa sikukuu.

Mkapa anasema imani kuwa mtu mwenye chombo cha moto ana fedha, si jambo la kiungwana kuwadai rushwa.

Anakiri kuwa wakati anaingia madarakani hali ya rushwa ndio ilikuwa mbaya kutokana na mishahara kuwa midogo na pia ilikuwa inachelewa kulipwa kwenye sekta ya umma.

“Matokeo yake watu wakawa wanabanwa kutoa rushwa ili kupata huduma ambazo ni haki yao kama zile za hospitali, elimu na hata yakija masuala ya kupata maji,” anaeleza Mkapa.

Mkapa anasema baada ya tume ya Warioba kutoa ripoti yake ya namna ya kupambana na rushwa, alianza kuchukua hatua kama kuimarisha Taasisi ya Kuzuia Rushwa (Takuru) na kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mwaka 2007 baada ya kuondoka madarakani.

Mkapa anafichua hali hiyo ya kusuasua kwa chombo hicho ilitokana na tatizo la kutoelewana kwa viongozi wake wa juu.

Mkuregenzi mkuu wa Takuru wakati huo alikuwa marehemu Meja Jenerali Anatory Kamazima na naibu wake akiwa, Edward Hoseah.

Mkapa anasema Kamazima na Hoseah walikuwa wana tofauti zao zilizodhoofisha utendaji wa taasisi yenyewe.

Anasema kutokana na hali hiyo taasisi hiyo haikuweza kuwa na ufanisi katika mapambano ya kutokomeza rushwa nchini.

Advertisement