Mke wa mfanyabiashara Hariri aunganishwa kesi ya dawa za kulevya

Muktasari:

Mfanyabiashara Hariri Mohamed Hariri na mkewe Muna Omary Saidi wameunganishwa katika kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa gramu 214.11

 


Dar es Salaam. Mfanyabiashara Hariri Mohamed Hariri na mkewe Muna Omary Saidi wameunganishwa katika kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa gramu 214.11.

Washtakiwa hao waliunganishwa katika kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu leo Alhamisi Agosti 22,2019 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi ambapo wanakabiliwa na shtaka la kusafirisha dawa za kulevya.

Awali, Hariri alisomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Mtega ambapo shauri hilo upelezi wake ulikamilika na alisomewa maelezo ya awali (PH) na kesi hiyo ilipelekwa katika Mahakama Kuu Kitengo cha mafisadi.

Wakili wa Serikali Faraja Nguka aliwasomea mashtaka hayo alidai walitenda kosa hilo Machi 2,2018 maeneo ya Kinondoni Matitu, Dar es Salaam.

Nguka alidai kwa pamoja walisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin gramu 214.11 huku upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa kutajwa.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Mwaikambo alisema washtakiwa hao hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo na aliahirisha hadi Septemba 5,2019.