Mkurugenzi Mwanga ashindwa kujibu swali, RC Mghwira aagiza asilipwe mshahara

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,  Anna Mghwira amemshukia mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Mwanga,  Zefrin Lubuva na kutaka mamlaka  yake kutomlipa mshahara wa mwezi Februari, 2020 hadi atakapobadilika.

Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,  Anna Mghwira amemshukia mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Mwanga,  Zefrin Lubuva na kutaka mamlaka  yake kutomlipa mshahara wa mwezi Februari, 2020 hadi atakapobadilika.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Februari 14, 2020  baada ya mkurugenzi huyo kushindwa kujibu swali alilomuuliza katika kikao maalumu cha kamati ya ushauri ya Mkoa huo kuhusu

halmashauri hiyo kushindwa kutoa asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

"Mkurugenzi naomba kupata taarifa ya makusanyo yenu na kiasi mlichotoa kwa vikundi vya kina mama, vijana na watu wenye ulemavu, mmetoa kwa asilimia ngapi na kwa nini hamjafikia malengo kama Serikali ilivyoelekeza, “ amesema  Mghwira.

Baada ya swali hilo, mkurugenzi alipewa kipaza sauti ili kujibu lakini alitaka ajibu mtaalamu mwingine jambo ambalo Mghwira alilipinga na kutaka ajibu mwenyewe.

Licha ya kutakiwa kujibu Lubuva alishindwa na kunyamaza kimya na kumfanya mkuu huyo wa Mkoa kumtaka mwenyekiti wa halmashauri hiyo kujibu.

Mwenyekiti wa Halmashauri,  Theresia Msuya amesema kutofikia malengo kumetokana na uzembe wa watendaji.

Baada ya maelezo hayo,  Mghwira  alimtaka tena Lubuva kusimama na kutoa majibu  kwa nini hawajafikia lengo la kutoa asilimia 10 kama Serikali inavyoelekeza lakini kwa mara ya pili alishindwa kujibu.

"Mkuu naomba radhi tugange yajayo" amesema  Lubuva na kisha kuketi.

"Sasa wanaokulipa mshahara wasikulipe mwezi huu, tugange yajayo mpaka huo mwezi Machi,” amesema mkuu huyo wa Mkoa.

Mghwira amezitaka halmashauri za wilaya kuhakikisha zinatekeleza maelekezo ya Serikali ya kutoa asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya vikundi vya kina mama, vijana na watu wenye ulemavu.

Halmashauri ya Mwanga hadi kufikia Januari, 2020 ilikuwa imetoa Sh17 milioni kwa vikundi vya wanawake na hakuna kikundi cha vijana wala walemavu kilichopewa  fedha hizo.