VIDEO: Mkurugenzi wa JamiiForums ahukumiwa kulipa faini ya Sh3 milioni

Muktasari:

Mahakaka ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu, Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa JamiiForums, Maxence Melo(40) kulipa faini ya Sh3 milioni au kwenda jela mwaka mmoja, baada ya kutiwa hatiani katika shtaka moja la kuzuia jeshi la polisi kufanya uchunguzi.
Pia mahakama hiyo imemuachia huru Micke Mushi ambaye ni mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo ya jinai namba 456/2016.

Dar es Saalm. Mahakaka ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu, Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa JamiiForums, Maxence Melo(40) kulipa faini ya Sh3 milioni au kwenda jela mwaka mmoja, baada ya kutiwa hatiani katika shtaka moja la kuzuia jeshi la polisi kufanya uchunguzi.

Pia mahakama hiyo imemuachia huru Micke Mushi ambaye ni mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo ya jinai namba 456/2016.

Mushi ameachiwa huru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha shtaka dhidi yake.

Uamuzi huyo umetolewa leo Jumatano Aprili 8, 2020 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakamani hiyo, Thomas Simba wakati kesi hiyo lilipoitwa kwa ajili ya hukumu.

"Mahakamani hii imemtia hatiani Mello kama alivyoshtakiwa hivyo atalipa faini ya Sh3 milioni au kwenda jela mwaka mmoja," amesema Hakim Simba na kuongezea

"Pia mahakama hii baada vya kupitia ushahidi wa mashahidi wanne wa upande wa mashtaka, umeona kuwa  mshtakiwa wa pili katika kesi hii Meck William Mushi hakuna ushahidi wowote uliomuonyesha kuwa ni Mkurugenzi wa Kampuni ya JamiiMedai, hivyo mahakama hii inamuachia huru mshtakiwa huyu," amesema Hakimu Simba.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Silvia Mitanto aliomba mahakama hiyo itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo.

"Naiomba mahakama itoe adhabu kali sana itakayomfanya mshtakiwa ajutie adhabu hiyo, ambayo itakuwa ni fundisho kwa jamii nzima, ili jamii ijue inahitaji ushirikiano kwa jeshi la polisi pale inapohitajika," alisema Mitanto.

Kwa upande wa Wakili wa utetezi, Peter Kibatala akisaidiana na Benedict  Ishabakaki na Jebra Kambole walisema kuwa mshtakiwa ni mkosaji wa kwanza hivyo anaomba apewe adhabu nafuu ya faini.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kuzuia jeshi la polisi kufanya uchunguzi, kinyume na Sheria Namba 22 (2) cha Sheria ya Makosa ya Mtandano Namba 14 ya mwaka 2015.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo, kati ya Aprili Mosi, 2016 na Desemba 13, 2016  katika maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni.