Mkurugenzi wa zamani Wizara ya Habari kizimbani kwa tuhuma kuchota Sh11 milioni

Tuesday August 20 2019

ubadhilifu na ufujaji wa fedha,Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Easter Liwa,Pascal Magabe,

 

By Pamela Chilongola,Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Aliyekuwa mkurugenzi msaidizi wa maendeleo wa vijana Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Easter Liwa amepandishwa kizimbani akikabiliwa na mashtaka 24.

Liwa amefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumanne Agosti 20, 2019 akikabiliwa na mashtaka hayo, likiwemo la kutengeneza nyaraka za uongo zenye thamani ya Sh11.1 milioni.

Akisomewa mashtaka na wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Pascal Magabe, amedai  kati ya mashtaka hayo 22 ya kughushi, moja la kutumia nyaraka ya kumdanganya mwajiri wake, ubadhilifu na ufujaji wa fedha.

Katika  shtaka la kwanza hadi la 16, inadaiwa kati ya Machi 11, 2015 na Juni 30, 2015 katika Wizara hiyo mshtakiwa akiwa na nia ya uovu kwa kufahamu alitengeneza nyaraka ya uongo za orodha ya walipaji iliyoonyesha posho ya kujikimu maofisa wa wilaya yaliyofanyika mkoani Singida kuanzia Machi 11 hadi 19, 2015.

Amesema alifanya hilo  kwa lengo la kuonyesha maofisa 16 waliohudhulia mafunzo ya uhamasishaji kwa vijana walilipwa posho ya Sh512,000.

Amedai kuwa katika shtaka la 17 hadi la 20 tarehe hiyo, mshtakiwa akiwa na nia ya uovu kwa kufahamu alitengeneza nyaraka ya uongo za orodha ya walipaji iliyoonyesha ”Posho ya waandishi wa Habari” kuanzia Machi 11 mpaka 19, 2015 kwa lengo la kuonyesha waandishi wanne wa radio ya Standard waliohudhulia kikao cha mafunzo ya uhamasishaji kwa vijana na walilipwa Sh1.1 milioni.

Advertisement

Katika shtaka la 25 tarehe hiyo  mshtakiwa akiwa na nia ya ovu kwa kufahamu alitengeneza nyaraka ya uongo ya Mwaju Shop iliyotumika kununulia vifaa vya ofisini vilivyotumika kwenye mafunzo ya uhamasishaji kwa vijana iliyogharimu  Sh250,000.

Magabe amedai  katika shtaka la 22,  Machi 17, 2015 alighushi risiti ya duka linalouza vifaa vya maofisini la Temo kwa lengo la kuonyesha Sh155,000 zilitumika kwenye gharama za mafunzo ya uhamasishaji kwa vijana.

Amedai kuwa dhtaka 23 kati ya Mei 25, 2015 katika ofisi za wizara hiyo mshtakiwa  akiwa na nia ya kumdanganya mwajiri wake alitengeneza nyaraka za uongo inayoitwa Marejesho ya Masurufu Maalumu iliyogharimu Sh11.1 milioni ambayo ilitumika katika mafunzo ya uhamasishaji kwa vijana huku akijua siyo kweli.

Katika shtaka la 25 kati ya Machi 11,2015 na Juni 30,2015 katika ofisi za wizara hiyo mshtakiwa huyo akiwa na nia ovu alifanya ubadhilifu wa fedha kiasi cha Sh5.4 milioni ambayo alikabidhiwa na wizara hiyo kwa ajili ya mafunzo ya uhamasishaji kwa vijana.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo mshtakiwa alikana makosa yanayomkabili na upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea.

Magabe amedai kuanzia shtaka la 25 hadi la 31 linamuhusu mshtakiwa Richard Msey ambaye hakuwepo mahakamani hapo hivyo aliiomba mahakama hiyo itoe hati ya kukamatwa.

Hakimu Mkazi Vick Mwaikambo amesema dhamana ipo wazi,  wanatakiwa wadhamini wawili wanaotoka kwenye ofisi yeyote inayotambulika watakaosaini bondi ya Sh30 milioni. Mshtakiwa alishindwa kukidhi masharti ya dhamana amerudishwa rumande hadi Septemba 3, 2019 kesi hiyo itakapotajwa.


Advertisement