Mkutano wa Twaweza, waandishi wa habari waahirishwa

Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze

Muktasari:

Mkutano wa waandishi wa habari nchini Tanzania ulioandaliwa na taasisi ya Twaweza Afrika Mashariki kuzungumzia siku ya kimataifa kupinga ukatili dhidi ya wanahabari duniani umeahirishwa.

Dar es Salaam. Mkutano wa waandishi wa habari nchini Tanzania ulioandaliwa na taasisi ya Twaweza Afrika Mashariki kuzungumzia siku ya kimataifa kupinga ukatili dhidi ya wanahabari duniani umeahirishwa.

Mkutano huo uliokuwa ufanyike leo Ijumaa Novemba Mosi, 2019 umeahirishwa bila kutajwa sababu.

Taarifa ya kuahirishwa kwa mkutano huo uliokuwa ufanyike katika ofisi za taasisi hiyo Kinondoni, jijini Dar es Salaam imetolewa na mkurugenzi wa Twaweza,  Aidan Eyakuze saa 4:00 asubuhi muda uliotakiwa uanze.

“Kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu hatutaendelea na mkutano,” amesema Eyakuze kwa ufupi.

Licha ya Mwananchi kuhoji sababu za kuahirishwa kwa mkutano huo, Eyakuze hakutaka kuzungumza zaidi.

Mmoja wa maofisa wa taasisi hiyo kwa sharti la kutotajwa jina lake amesema kuna zuio limetolewa bila kuweka wazi aliyelitoa.

Siku mbili kabla ya mkutano huo, Twaweza walisambaza tangazo la mkutano huo kupitia mitandao ya jamii, “Tunakualika katika mkutano na wana habari katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya kupinga ukatili dhidi ya wana habari duniani.”