Mkuu wa kanisa KKKT kuchaguliwa Agosti 23

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheri (KKKT),Dk Fredrick Shoo(kushoto) akizungumza jambo na Askofu Dayosisi ya Kaskazini Mashariki,Dk Steven Munga wakati wa mkutano Mkuu wa 20 wa Kanisa hilo unaofanyika katika Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira mkoani Arusha leo.Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

Ijumaa Agosti 23, 2019 wajumbe wa halmashauri kuu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) watamchagua mkuu wa kanisa hilo atakayeliongoza kwa miaka minne ijayo

 


Arumeru. Ijumaa Agosti 23, 2019 wajumbe wa halmashauri kuu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) watamchagua mkuu wa kanisa hilo atakayeliongoza kwa miaka minne ijayo.

Mkuu wa Kanisa hilo hivi sasa, Askofu Dk Fredrick Shoo amemaliza muhula wa kwanza wa miaka minne na wajumbe hao wanaweza kumwongezea muhula wa mwisho au kumchagua mwingine.

Leo Jumanne Agosti 20, 2019 wajumbe hao wameanza kikao cha ndani ikiwa ni sehemu ya mkutano mkuu wa 20 wa kanisa hilo.

Ratiba ya mkutano huo inaonesha ibada ya ufunguzi itafanyika leo saa 10 jioni na kuongozwa na Dk Shoo pamoja na maaskofu kutoka Dayosisi zote 26 nchini.

Rais wa Fungamano la Makanisa ya Kirutheri duniani, Dk Panti Filibus Musa atakua mzungumzaji mkuu katika siku tatu kuanzia kesho Jumatano,  pia ripoti mbalimbali kutoka dayosisi hizo zitawasilishwa.