Mkuu wa JKT ataja siri ya kuteuliwa na Magufuli

Muktasari:

Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) nchini Tanzania, Brigedia Jenerali Charles Mbuge ametaja sababu ya Rais wa Tanzania, John Magufuli kumteua kushika wadhifa huo.

Dar es Salaam. Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) nchini Tanzania, Brigedia Jenerali Charles Mbuge ametaja sababu ya Rais wa Tanzania, John Magufuli kumteua kushika wadhifa huo.

Amesema siri ya kuaminiwa ni kauli mbiu yake ya ‘maneno si kazi,  kazi ni vitendo’.

“Kauli hii imenisaidia katika utendaji wangu na nimeaminiwa na kupewa madaraka. Namshukuru sana (Rais Magufuli) kwa hiyo  ni vyema mkaitumia katika utendaji wenu,” amesema huku akisisitiza  ushirikiano kwa makamanda wa jeshi hilo.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Oktoba 23, 2019 baada ya kukutana kwa mara ya kwanza na makamanda hao tangu alipoteuliwa Septemba 10, 2019.

Mkutano huo uliwahusisha  makamanda wa vikosi na wakuu wa kanda.

“Tujipange kufanya kazi katika maeneo yote mliyoteuliwa ili mtimize malengo na jitihada za wanaotegemea katika nchi yetu kwamba tutafanya kazi,” amesema Brigedia Jenerali Mbuge.

Amewataka walio chini yake kutekeleza shughuli za uzalishaji mali ili kukidhi mahitaji na malezi ya vijana na  kutoa mchango katika Pato la Taifa.