Mkuu wa Mkoa Arusha aviomba vyombo vya habari kusaidia kukuza Utali

Mkuu wa wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe akifungua kongamano la Utalii la wanahabari kanda ya Kaskazini, kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Arusha,Mrisho Gambo.
Picha Husna Issa.

Muktasari:

  • Waandishi wa habari za Maliasili na Utalii kanda ya kaskazini wamekuwa wakikutana kila mwaka katika kongamano la Utalii kujadili mchango wa vyombo vya habari katika kukuza Utalii.

Arusha. Mkuu wa Mkoa Arusha, Mrisho Gambo amewataka  Waandishi wa habari kusaidia kukuza sekta ya utalii kwa kuandika habari nzuri  na kuacha mabaya, ili kuvutia watalii.

Gambo ametoa ombi hilo jana jioni, wakati akifungua kongamano la tatu la Utalii la Arusha Tourism Festival,  lilikuwa limeandaliwa na waandishi wa habari za Utalii kwa kushirikiania na Taasisi ya Arusha Media na waandishi kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara.

Katika yake Gambo iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe, amesema vyombo vya habari vina fursa nzuri ya kukuza utalii nchini Tanzania.

Amesema Mkoa wa Arusha unabeba dhamana ya utalii kwa zaidi ya asilimia

73, ukilinganisha na mikoa mingine nchini, hivyo wanahabari lazima wajikite kuandika habari nzuri za sekta hiyo ili kuisaidia.

“Wanahabari mnabeba dhamana kubwa katika kutangaza vivutio vyetu, lakini mnapoandika habari mbaya za sekta hii, mnatoa mwanya kwa washindani wetu kuzisambaza kwa nguvu habari hizo ili tusipate watalii,” amesema Gambo.

Amesema ili mtalii aje nchini, lazima ajihakikishie usalama wake, mali zake na hivyo kumlazimu kutafuta taarifa za nchi husika atakayoenda.

“Sasa kama mkiandika kuna maandamano, ghasia na vinginevyo washindani

wetu watasambaza taarifa hizo kwa nguvu ili wapate watalii wao na sisi

tukose, hivyo ni vema tushiriki wote kutangaza mema tu ya Taifa letu, ili

tukuze zaidi sekta hii,” amesema Gambo.

Amesema Serikali inapambana kuhakikisha sekta hii inakua na ndio maana imenunua ndege, kwa ni unapokua na usafiri wa uhakika ni moja ya njia ya kuongeza watalii.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC) Claud

Gwandu, amesema ni vema wanahabari nchini, wakabadilika katika

uandishi wa habari za sekta ya utalii.

“Ili mtalii aje Tanzania, ni lazima tuwe na kitu cha ziada na kitu hicho siyo kingine ni amani, kwa sababu kama wanyama Simba,Twiga,Tembo, Mbogo na

wengine nao wapo nchi jirani, sasa sisi tunawajibu wa kutangaza amani

tuliyonayo kwa nguvu zetu zote,” amesema.

Mkurugenzi wa Taasisi ya wanahabari ya Arusha Media, Mussa Juma amesema  kongamano hilo linafanyika kila mwaka, likilenga kuongeza ari kwa wanahabari ya kuandika zaidi na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

“Lakini pia taasisi hii inalenga kujenga uwezo kwa wanahabari, jinsi ya kupiga vita ujangili na kutumia kalamu zao kuhamasisha utalii wa ndani,” alisema.

Nao viongozi wa chama cha mawakala wa Utalii nchini Tanzania (Tato), Chama cha Wawindaji wa Kitalii (Tahoa) na Chama cha Wapagazi wa Mlima Kilimanjaro (TPO), wote walisema vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kukuza sekta hiyo.

Kongamano hilo ambalo pia lilishirikisha wanafunzi wa vyuo vya uandishi wa habari, lilidhaminiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa),Taasisi ya Chemchem Association na Mfuko wa Uhifadhi wa Friedkin (FCF).