Mkuu wa mkoa Mnyeti afunga migodi ya madini ya ujenzi

Wednesday October 9 2019

By Joseph Lyimo, Mwananchi [email protected]

Simanjiro. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, ameyasimamisha kwa muda machimbo ya madini ya ujenzi ya Losinyai Kata ya Oljoro namba 5 Wilayani Simanjiro, baada ya wapakiaji mchanga kulalamikia kulipwa ujira mdogo.

Mnyeti ametoa agizo hilo leo Jumatano Oktoba 9, 2019 baada ya wapakiaji wa mchanga kwenye malori kulalamikia kulipwa ujira mdogo na kisha kutembelea machimbo hayo.

Amesema anayafunga kwa muda machimbo hayo na kumuagiza mkuu wa Wilaya hiyo, Zephania Chaula kukaa na wapakiaji mchanga kwenye migodi hiyo na wenye malori ili kufikia mwafaka.

"Hamuwezi kuwalipa Sh24,000 au Sh26,000 hawa wapakiaji, walipeni Sh35,000 kama sehemu nyingine wanavyolipa, mkuu wa wilaya simamia hilo," amesema Mnyeti.

Pia, ameagiza baadhi ya viongozi kwenye migodi ya machimbo hayo ya madini ya ujenzi ya mchanga (masteling) kutoshirikishwa kwenye shughuli hiyo.

"Mtu wa kati anayeitwa ‘steling’ sitaki kumuona kwa sababu anatumika kuwanyonya wapakiaji mchanga hawa, kwa hiyo wenye malori waonane moja kwa moja na wapakiaji," amesema Mnyeti.

Advertisement

Amemuagiza pia Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, kuyafungua machimbo hayo baada ya kukutana na wahusika hao ili utekelezaji huo ufanyike.

Baadhi ya wapakiaji wa mchanga kwenye malori yanayobeba mchanga huo wamepongeza hatua hiyo iliyochukuliwa na mkuu wa mkoa Mnyeti.

Mmoja wa wapakiaji mchanga, Ally Ramadhan amesema mkuu huyo wa mkoa amesikilia kilio chao na kutoa agizo lake limekuja kwa wakati mwafaka.

“Tumeteseka kwa muda mrefu kwa kulipwa ujira mdogo na pia wenye malori huwa wanakuja na wapakiaji mchanga wao kutoka Arusha," amesema Ramadhan.

Madini ya ujenzi ya mchanga ya Losinyai Wilayani Simanjiro yanatumika kujenga majengo mengi jumba jijini Arusha na malori mengi hutoka Arusha kufuata madini hayo ambayo machimbo yake mengine yapo mpakani mwa wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.

 

 


Advertisement