Mkuu wa shule adakwa mkutanoni akidaiwa kumwomba rushwa ya ngono mwanafunzi

Sosthenes Kibwengo 

Muktasari:

Mkuu wa Shule ya sekondari Serengeti wilayani Serengeti mkoani Mara, Baraka Sabi aliyekuwa Dodoma akihudhuria mkutano wa waalimu wakuu alikamatwa na Takukuru kwa kosa la kumuomba rushwa ya ngono aliyekuwa mwanafunzi wa shule hiyo

Dodoma . Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Dodoma, inamshikilia Mkuu wa Shule ya Sekondari Serengeti wilayani Serengeti mkoani Mara, Baraka Sabi kwa kosa la kutaka rushwa ya ngono kwa aliyekuwa mwanafunzi wa shule hiyo.

Mkuu wa Taasisi hiyo Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo leo Desemba 15, 2019 Jijini hapa amewaambia waandishi wa habari kuwa mtuhumiwa huyo alitaka rushwa ya ngono kama sharti la kumpatia mtoa taarifa cheti chake cha kuhitimu kidato cha sita.

Kibwengo amesema kuwa mtoa taarifa alikuwa akiwasiliana na mtuhumiwa ili kupata cheti hicho, ambapo mwalimu huyo alishauri aje na cheti hicho kwani ana safari ya kuja Dodoma kuhudhuria mkutano wa wakuu wa shule za sekondari ili kumpunguzia gharama za kusafiri hadi shuleni.

Amesema mtoa taarifa aliwaambia kuwa baada ya kufika ili kuchukua cheti chake mwalimu huyo alihitaji kupewa rushwa ya ngono ili atoe cheti ambapo mtoa taarifa aliomba udhuru na kuahidi kurejea siku uliyofuta.

"Desemba 12, 2019 tulipokea taarifa kutoka kwa msichana (jina limehifadhiwa) mkazi wa jiji la Dodoma ambaye alihitimu kidato cha sita katika shule hiyo mwaka 2016 na kwamba mtuhumiwa amemtaka kingono ili mpatie cheti kwa ajali ya maombi ya ajira baada ya kuhitimi chuo kikuu," amesema Kibwengo.

Amesema baada ya kupokea taarifa hiyo waliweka mtego na kufanikiwa kumkamata akiwa na mtoa taarifa kabla yakufanya tendo hilo.

Amesema Takukuru walifanikiwa kuchukua cheti hicho na uchunguzi wa awali unaendelea kwa mujibu wa sheria na hatua stahiki zitachukuliwa baada ya kukamilika.