Mkuu wa wilaya ya Chemba afungua kesi, ataka kuwataliki wake zake wawili

Mkuu wa Wilaya ya Nchemba Ezekiel simon Odunga  akiwa katika mahakama ya Mwanzo Ukonga akisuburi kuingia mahakamani katika kesi ya madai ya takala aliyoifungua dhidi ya mkewe Ruth Osoro. Na Mpiga Picha Wetu

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga amefungua kesi mbili za madai ya talaka kwa wake zake wawili katika Mahakama ya Mwanzo ya Ukonga.

Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga amefungua kesi mbili za madai ya talaka kwa wake zake wawili katika Mahakama ya Mwanzo ya Ukonga.

Katika kesi moja ya kesi hizo ambayo ni ya madai namba 180 ya 2019, iliyo mbele ya Hakimu Elia Mrema, Odunga anaomba talaka dhidi ya ndoa ya Serikali aliyofunga Februari 21, 2010 na Ruth Osoro.

Pia, anaomba apewe ridhaa ya kumlea mtoto wao wa kiume wa miaka minne bila bughudha yoyote.

Mbali na kesi hiyo dhidi ya Ruth ambayo itasikilizwa Agosti 19, Odunga pia atakuwa mahakamani hapo Julai 30 katika kesi nyingine ya mwaka 2019 dhidi ya ndoa aliyoifunga kanisani na mwanamke mwingine.

Katika kesi dhidi ya Ruth, Odunga anaomba kutoa talaka kwa mkewe huyo kwa sababu amechoshwa na ugomvi na kudhalilishwa sehemu zake za kazi ingawa aliieleza Mahakama kuwa hana shaka na malezi ya mama wa mtoto huyo ila anataka amlee mtoto wake ili aweze kuepuka kadhia ya kudhalilishwa kila mahali ikiwamo kazini.

Alidai kuwa wakati anamuoa alikuwa akitambua kwamba ana mwanamke mwingine lakini alikuwa hajafunga naye ndoa na kwamba alimuoa kwa kuwa walikuwa na mgogoro wa kifamilia na Ruth aliridhia hilo.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa cheti hicho cha ndoa kinaonyesha kuwa wakati wanaoana, Odunga alikuwa hajaoa na Ruth alikuwa hajaolewa na alitoa nakala ya cheti hicho mahakamani hapo.

Kwa upande wake Ruth, alipinga kutolewa kwa talaka akisema bado anampenda mumewe na anataka mtoto wake alelewe na wazazi wote.

Hata hivyo, aliiambia mahakama kuwa licha ya manyanyaso aliyopitia kutoka kwa mumewe huyo, kutelekezwa na mwanaye kwa miaka mitatu bila ya kupewa matumizi, amemsamehe.

 

Kwa habari zaidi soma gazeti la Mwananchi la leo Jumamosi Julai 27, 2019