Mmiliki wa PSG akataa kujibu maswali 28 ya waendesha mashtaka

Muktasari:

Tajiri huyo wa Qatar aliamua kukaa kimya kila alipoulizwa swali na waendesha mashtaka kuhusu tuhuma za rushwa katika utoaji wa wenyeji wa mashindano ya ubingwa wa dunia wa riadha kwa taifa hilo.


Paris, Ufaransa (AFP). Mmiliki wa klabu ya Paris Saint-Germain, Nasser Al-Khelaifi aliamua kukaa kimya wakati akihojiwa na waendesha mashtaka wa Ufaransa kuhusu maombi ya Doha kuandaa michuano ya ubingwa wa dunia wa riadha, kwa mujibu wa nyaraka ambazo AFP imeziona.

"Natumia haki yangu ya kukaa kimya," alijibu kiongozi huyoo raia wa Qatar kila alipoulizwakati ya maswali 28 aliyopewa Juni 11 jijini Paris.

Alishtakiwa mwezi Mei akihusishwa na maombi ya jiji la Doha kuwa mwenyeji wa michuano hiyo mikubwa ya riadha.

Mji huo mkuu wa Qatar ulizidiwa kete na London mwaka 2017 lakini ukaibuka kidedea mbele ya Eugene na Barcelona kuandaa michuano ya mwaka huu, ambayo ilifanyika kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Khalifa kati ya Septemba 27 nad Oktoba 6.

Wanasheria wake, Francis Szpiner na Renaud Semerdjian waliiambia AFP kuwa mteja wao alikataa kutoa ushirikiano kwa kuwa "majibu yote muhimu yalishatolewa".

"hakukuwa na kitu kipya tangu mahojiano ya mwisho," walisema.

Al-Khelaifi, ambaye pia ni mmiliki wa televisheni ya Qatar ya BeIN Sports, alifunguliw amashtaka mwezi Mei. Alishindwa kuhudhuria wito wa kwanza wa mahojiano na waendesha mashtaka mwezi huo kwa sababu alikuwa Qatar katika fainali ya michuano ya mtoano.

Waendesha mashtaka wa Ufaransa wanachunguza miamala miwili ya malipo ya dola 3.5 milioni za Kimarekani yaliyofanywa mwaka 2011 na Oryx Qatar Sports Investment, kampuni inayoendeshwa na kaka wa Nasser anayeitwa Khalid Al-Khelaifi, kwenda kwa kampuni ya masoko inayoendeshwa na Papa Massata Diack.

Baba yake Diack anayeitwa Lamine Diack alikuwa rais wa Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF) kuanzia mwaka 1999 hadi 2015 na mjumbe wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC).

Al-Khelaifi amekana kuhusika na makosa yoyote.