VIDEO: Mmiliki wa hoteli aeleza kilichotokea kwa mfanyabiashara wa Mwanza anayedaiwa kumpiga risasi mpenzi wake

VIDEO: Mmiliki wa hoteli aeleza kilichotokea kwa mfanyabiashara wa Mwanza anayedaiwa kumpiga risasi mpenzi wake

Geita. Mkurugenzi wa Hoteli ya Kilimanjaro mkoani Geita ameeleza jinsi walivyosikia risasi ilikia katika chumba alichokuwa mfanyabiashara wa jijini Mwanza Salum Othuman (44) ambaye anadaiwa kumpiga risasi mpenzi wake kwa kwa kile kinachodaiwa ni wivu wa mapenzi.

Mkurugenzi huyo Paul Lyimo akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Februari 27, 2020 amesema mtuhumiwa ni mteja wao wa mara kwa mara na kwamba asubuhi akiwa chumbani wahudumu walisikia mlio wa risasi na ghafla alitoka chumbani akiwa amembeba Happynes Israel huku damu ikiwa inachuruzika.

“Alipotoka meneja alikuwa akimzuia asiondoke akamtolea bastola kumtisha meneja akarudi nyuma ndipo aliporudi nyuma akagonga geti na kumgonga meneja kisha kumburuza ndio vijana wa bodaboda hapo nje wakaanza kumkimbiza akawa anakimbia na gari barabara kuu kuelekea Mwanza na alipofika mbele ya soko la dhahabu alizunguka na kushuka eneo la hospitali na kufanikiwa kukamatwa na polisi,” amesema Lyimo.

Kaimu mganga mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Geita, Shaban Masawe alikiri kupokea majeruhi wawili wa tukio hilo ambapo amesema Happines alipigwa risasi eneo la paja na uchunguzi umeonyesha amevunjika mfupa na amepewa rufaa ya kwenda hospitali ya Bugando huku mwingine akiwa na michubuko maeneo mbalimbali ya mwili wake.