Jimbo la Moshi mjini laangukia CCM baada ya miaka 25 ya kuwa Chadema

Muktasari:

Jimbo la Moshi mjini limekuwa chini ya upinzani tangu uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi 1995, lakini safari hii mgombea wa CCM, Priscus Tarimo ameitoa CCM kimasomaso kwa kushinda uchaguzi huo.

 

Moshi. Imewezekana safari hii, ndivyo unavyoweza kuelezea matokeo ya ubunge Jimbo la Moshi mjini baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kulitwaa jimbo hilo baada ya kulisaka kwa kwa miaka 25 mfululizo tangu uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi 1995.

Jimbo la Moshi mjini na lile la Karatu ndio majimbo pekee yaliyokuwa chini ya upinzani tangu uchaguzi mkuu huo, lakini  katika uchaguzi mkuu wa 2020, CCM kimevunja uteja kwa upinzani kwa kuweza kulikomboa Jimbo la Moshi mjini.

Katika matokeo yaliyotangazwa leo Oktoba 29,2020 na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Michael Mwandezi, mgombea ubunge wa CCM, Priscus Tarimo ameibuka na ushindi kwa kupata kura 31,169 huku mshindani wake wa karibu, Raymond Mboya wa Chadema akipata kura 22,555.

Mwandezi alisema katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, jimbo la Moshi mjini lilikuwa na wapiga kura walioandikishwa 143,267 na waliopiga kura walikuwa 54,994 ambapo kura halisi zilikuwa 54,386 na kura 608 ziliharibika.

Wagombea wengine wa ubunge katika jimbo hilo na kura zao zikiwa kwenye mabano ni Buni Ramole wa ACT-Wazalendo (374), Issack Kireti wa SAU(93), Fatuma Msuya wa Cuf (85), Dk Godfrey Malisa wa NCCR-Mageuzi (59) na Neema Mushi wa Demokrasia Makini (51).

Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Priscus aliahidi kwenda kutekeleza ahadi mbalimbali za maendeleo alizozitoa kwa wananchi wa jimbo hilo na kuwashukuru wapiga kura wa jimbo hilo kwa kumwamini na kumpa ridhaa.

Historia inaonyesha uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi 1995, Jimbo la Moshi lilichukuliwa na Joseph Mtui wa NCCR-Mageuzi na baadae akaja Ndesamburo (2000-2015) na kurithiwa na Jaffar Michael wa Chadema pia.

Ndesamburo ambaye alikuwa mmoja wa waasisi wa Chadema na mfadhili wa chama, alikuwa na kadi ya uanachama namba 10 na ndiye alikuwa mwiba na alikuwa na uwezo wa kuvuruga mipango ya CCM.

Mara zote alitamba hakuna mtu wa kuweza kumng’oa mpaka atake mwenyewe na ndivyo ilivyotokea mwaka 2015 ambapo alimtangaza mrithi wake (Jaffar) mapema na akawashawishi wananchi wamkubali.

Kwa upande wake, mwaka 1995 Dk Willibroad  Slaa alishinda kura ya maoni ndani ya CCM lakini badala yake, jina la Patrick Qorow ndio likarudishwa na wananchi wakamuomba ahamie chama chochote watampa kura.

Dk Slaa akahamia Chadema na kupitishwa kuwa mgombea Ubunge ambapo alishinda na kuwa Mbunge tangu 1995 hadi 2010 alipoachia na kuamua kwenda kugombea Urais akichuana na Jakaya Kikwete.

Mchungaji Israel Natse wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), akamrithi Dk Slaa, lakini akahudumu kwa miaka mitano tu hadi 2015 na viatu vyake kuvaliwa na Willy Qambalo wa Chadema.