Mpoto ataka wasanii kutovaa viatu kongamano la Nyerere

Muktasari:

  • Msanii wa kughani mashairi nchini Tanzania, Mrisho Mpoto amewaomba wenzake watakaohudhuria kongamano la kumuenzi mwalimu Julius Nyerere kutovaa viatu.

Dar es Salaam. Msanii wa kughani mashairi nchini Tanzania, Mrisho Mpoto amewaomba wenzake watakaohudhuria kongamano la kumuenzi mwalimu Julius Nyerere kutovaa viatu.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Novemba 14, 2019 katika mkutano kueleza yatakayojiri kwenye kongamano hilo litakalofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).

Amesema kutovaa viatu kutawafanya wasanii kumkumbuka vyema Nyerere aliyefariki dunia Oktoba 14, 1999.

"Kwangu kufanyika kwa tamasha kama hili naona tunaenda kumfufua tena kiongozi wetu mwenye mchango mkubwa katika Taifa na kuonyesha namna gani ni shujaa wetu, lazima  tumuenzi kwa staili yake," amesema  Mpoto.

Awali, katibu mtendaji wa bodi ya filamu, Dk Kiagho Kilonzo amesema wazo la kufanya shughuli hiyo lilikuwa la watu wachache lakini wadau wengi walishiriki na kulifanya kuwa kubwa.

Kaimu mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Onesmo Kayanda amesema mwalimu Nyerere amefanya mengi ambayo baadhi yanafanywa kwa sasa na Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Katika kongamano hilo tuzo zitatolewa kwa familia ya mwalimu Nyerere, Rais Magufuli na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.