Mradi soko la Kijichi kuzinduliwa, wafanyabiashara kuwekewa majokofu

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke wa pili kushoto, Lusubilo Mwakibibi akielelekezwa na Mratibu wa Miradi ya Maendeleo jiji la Dar es Salaam wa Halmashauri hiyo, Simon Edward.Picha na Pamela Chilongola

Muktasari:

  • Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Lusubilo Mwakibibi amesema Septemba Mosi, 2019 watazindua miradi ya soko la Kijichi, Mbagala na Makangarawe yenye thamani zaidi ya Sh3 bilioni.

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Lusubilo Mwakibibi amesema Septemba Mosi, 2019 watazindua miradi ya soko la Kijichi, Mbagala na Makangarawe yenye thamani zaidi ya Sh3 bilioni.

Mwakibibi ametoa kauli hiyo leo Jumatano Agosti 21, 2019 alipotembelea miradi mbalimbali ya maendeleo jijini Dar es Salaam (DMDP) inayotekelezwa na halmashauri hiyo kwa mkopo wa Benki ya Dunia (WB).

Mwakibibi amesema Agosti 30, 2019 halmashauri ya manispaa hiyo watakabidhiwa masoko hayo ambayo kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 96.

“Mradi mwingine tutakaokabidhiwa ni stendi ya mabasi ya daladala Kijichi na Mbagala yenye thamani zaidi ya Sh1 bilioni, stendi hizo zipo maeneo yalipojengwa masoko haya yaani mtu akishuka tu hapati shida anaenda moja kwa moja kununua bidhaa anayotaka,” amesema Mwakibibi.

Mwakibibi amesema wananchi watatangaziwa utaratibu wa kufanya biashara katika masoko hayo ikiwemo kuomba maombi na watakapokamilisha watapewa vizimba hivyo ili wafanye biashara.

Amesema wafanyabiashara watakaokuwa katika soko la Kijichi watawekewa majokofu kwa ajili ya kuhifadhi nyanya zisiharibike.

Naye mratibu wa miradi ya DMDP wa manispaa hiyo, Simon Edward amesema katika soko la Kijichi kuna  vizimba 123, wanatarajia kuwa na wafanyabiashara 151 na soko la Mbagala lina vizimba 18 na Makangarawe vizimba 200.