VIDEO: VIDEO: Mrema aibuka, aidai fidia Serikali ya Mkapa

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP ) Augustine Mrema amezungumza na waandishi wa habari pamoja na mambo mengine ameitaka Serikali ya nchi hiyo inayoongozwa na Rais John Magufuli kumlipa Sh2 bilioni kama fidia ya kesi alizowahi kusingiziwa katika utawala wa awamu ya tatu.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema ameitaka serikali kumlipa Sh2 bilioni kama fidia ya kesi alizowahi kusingiziwa chini ya Serikali ya Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin Mkapa.

Mbali na hilo, anasema amemuandikia pia barua Rais John Magufuli ili kumweleza malalamiko yake juu ya aliyowahi kufanyiwa huku akiomba nafasi ya kuzungumza naye ili ampatie mbinu kuelekea uchaguzi mkuu 2020 na kuepusha yaliyotokea uchaguzi wa serikali za mitaa.

Aliyasema hayo jana katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam wakati akielezea hali ya kisiasa nchini.

Mrema ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, alisema kesi hizo zilikuwa zikitumika kama mbinu zilizokuwa zimelenga kumtoa katika ulingo wa siasa.

Alisema kwa sababu serikali imesema kumbambikia kesi mtu ni kosa la jinai ambalo wahusika wanatakiwa kukamatwa na kufikishwa mahakamani lakini muathirika anatakiwa kulipwa fidia hivyo ameomba Rais Magufuli kumlipa fidia kwa niaba ya serikali.

“Kwa kuwa nilibambikiwa na kuzushiwa kesi za uongo ambazo ni kosa kisheria, nakuomba Rais wa Tanzania (John Magufuli) na serikali yako mnilipe Sh2 bilioni kwani haya yote yalifanyika ili kukisaidia chama tawala na serikali yake ili kinishinde kisiasa,” alisema Mrema

“Hiyo hela ni ya chumvi na wasiponifidia nitawashtaki kwa wananchi na ninamuomba Rais Magufuli afute historia ya kuonewa kwa watu nchini na kuonewa kwangu,” alisema. Alisema kwa nyakati tofauti alibambikiwa kesi hizo ikiwemo ile ya kumuhusisha Rais mstaafu Mkapa na rushwa ya Sh500 milioni kauli aliyodaiwa kuitoa wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Temeke mwaka 1996 ambayo ilikosa ushahidi wa kumtia hatiani.

Muda mchache baadaye iliundwa kamati ya bunge ili kuchunguza nyaraka zilizokuwa zikihusisha tuhuma za rushwa dhidi ya vigogo mbalimbali wa serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambapo baada ya uchunguzi na mahojiano pia alibainika kuwa siyo yeye aliyetengeneza nyaraka hizo.

“Lakini hilo halikuishia hapo nilipewa tena kesi namba 61 ya mwaka 1999 wakidai nilitoa ushahidi wa uongo mbele ya kamati ya bunge,” alisema Mrema.

Alisema kitendo cha kupewa kesi hizo kilikuwa kikimuondolea imani kwa jamii inayomzunguka na kumuona mhuni au mtu muovu kutokana na kukamatwa na polisi.

“Sioni unafuu katika kunyamaza kwa sababu nchi hii ukiwa na nguvu wanaangalia namna ya kukudhoofisha kwa kutumia mbinu tofauti na hila kwa kutumia vyombo vyao,” alisema Mrema.

“Mengine nimevumilia sana mpaka basi, wapo wengine wanasema hakuna wa kuiondoa CCM madarakani ni kweli, inaondokaje kwa udhalimu huu na mtaji iliyonayo,” alisema Mrema

Alisema mbali na yale yaliyoandikwa katika barua ambayo Rais ataisoma ikiwemo malalamiko lakini anaamini kuna hatua ambazo atazichukua kwa sababu ni mtu mwema. “Kuna mambo mengine siwezi kumshauri hapa katika karatasi, nitakwenda kwake ana kwa ana ikiwemo lile la kuboresha uchaguzi mkuu ujao ninachotaka sasa barua yangu aisome, aipokee, aniite, yale ambayo sikuandika nimuambie na kama kuna mengine kuna haja ya kuitana atafanya hivyo.”

“Na sikufurahishwa na vitendo vilivyotokea katika uchaguzi wa serikali za mitaa jambo ambalo linaonyesha ni siasa gani tulizonazo hapa nchini kwani ni dhahiri walifanya mapinduzi ya wazi wazi,” alisema Mrema