Mrithi wa Tundu Lissu aapishwa bungeni, wabunge Chadema...

Mbunge wa Singida Mashariki (CCM), Miraji Mtaturu akila kiapo cha uaminifu mbele ya Spika wa Bunge jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Miraji Mtaturu ameapishwa leo Jumanne Septemba 3, 2019 kuwa mbunge wa Singida Mashariki (CCM) kuchukua nafasi ya Tundu Lissu (Chadema) aliyepoteza sifa za kuwa mbunge.

Dodoma. Miraji Mtaturu ameapishwa leo Jumanne Septemba 3, 2019 kuwa mbunge wa Singida Mashariki (CCM) kuchukua nafasi ya Tundu Lissu (Chadema) aliyepoteza sifa za kuwa mbunge.

Mtaturu ameapishwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai huku wabunge wa CCM wakimsindikiza kwa mbwembwe wakati wakiingia katika ukumbi wa Bunge.

Wakati mbunge huyo akila kiapo, eneo wanaloketi wabunge wa Chadema viti vilikuwa tupu.

Mara baada ya kuapishwa Mtaturu aliwapungia mkono wabunge waliokuwa katika ukumbi huo na kwenda kuketi.

Wakati Mtaturu akichukua nafasi yake, Ndugai amesema jimbo hilo sasa limepata mwakilishi halali.

Mtaturu ameapishwa baada ya jana Jumatatu Septemba 2, 2019 Mahakama Kuu nchini Tanzania kusema ombi la kusimamishwa kuapishwa kwake  haliwezi kutolewa.

Hayo yalielezwa saa 2:48 usiku na Jaji Sirillius Matupa  kuhusu maombi ya Lissu ya kibali cha kufungua shauri kupinga taarifa ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuhusu kukoma kwa ubunge wake.

Jaji huyo amesema kwenye kesi za ubunge hata kama mtu ameapishwa anaweza kuvuliwa ubunge pamoja na kiapo chake.

Jaji Matupa amesema maombi rasmi ya Tundu Lissu kupinga mambo kadhaa kuhusu kuondolewa katika ubunge yatatolewa Septemba 9, 2019.

Lissu amefungua maombi chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute  Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo, ikiwa ni hatua ya awali kabisa ya kupigania kurudishiwa ubunge wake.

Katika maombi hayo namba 18 ya mwaka 2019, dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Lissu anaomba kibali cha kufungua shauri la maombi maalum kwa lengo la kupata amri mbalimbali kuhusiana na uamuzi huo wa kuvuliwa ubunge.

Amri hizo kwa mujibu wa hati ya maombi na hati ya maelezo yake ni pamoja na Mahakama kumwamuru Spika wa Bunge awasilishe mahakamani taarifa ya kumvua ubunge aliyoitoa bungeni ili iweze kuupitia na kisha iamuru kuutengua na kuutupilia mbali.

Nyingine ni mahakama imwamuru Spika ampatie yeye Lissu nakala ya taarifa ya kumvua ubunge, amri ya  kusitishwa kuapishwa kwa Mtaturu

Mwanasheria mkuu huyo wa  Chadema yuko nchini Ubelgiji kwa ajili ya matibabu baada ya Septemba 7, 2017 kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajajulikana akiwa katika makazi yake, mjini Dodoma akiwa ametokea bungeni.

Juni 28, 2019 wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, Ndugai alitangaza kukoma kwa ubunge wa Lissu huku akisema si yeye aliyemvua ubunge bali ni matakwa ya katiba ya nchi.

Alitaja sababu za uamuzi huo kuwa ni kutohudhuria vikao vya Bunge kwa muda mrefu bila kumjulisha Spika kwa maandishi kueleza mahali alipo na kutotoa taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.