Mrithi wa Tundu Lissu ataka barabara ijengwe

Muktasari:

Mbunge wa Singida Mashariki Miraj Mtaturu ameitaka Serikali kujenga kwa haraka barabara ili kuinua pato la wananchi, asema yuko imara kuwatumikia wananchi wake.

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema iko mbioni kuanza ujenzi wa barabara ya Kuanzia Njiapanda (mkoani Singida) hadi Handeni (Mkoani Tanga).

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Alhamisi Septemba 12, 2019 na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa wakati ajibu swali la nyongeza na mbunge wa Singida Mashariki (CCM) Miraj Mtaturu.

Katika swali la nyongeza, Mtaturu ametaka kujua ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Njiapanda- Kwamtoro- Makiyungu hadi Handeni ambayo ina umuhimu katika uchumi wa wananchi wa maeneo hayo.

"Nakubaliana na Mheshimiwa Mtaturu kuwa barabara hiyo ina umuhimu mkubwa kwa wananchi, Serikali ilishamaliza michakato yote na sasa tunatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii yenye urefu wa kilomita 461," amesema Kwandikwa.

Barabara hiyo imekuwa ikiulizwa mara nyingi  bungeni ikitajwa kuwa muhimu kwa kuunganisha maeneo ya mikoa minne ya Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.

Mtaturu ni mbunge mpya wa jimbo hilo aliyechukua nafasi ya Tundu Lissu (Chadema) ambaye ubunge aliupoteza Juni 28, 2019 kwa kile kilichoelezwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai ni kutokutoa taarifa ya wapi alipo na kutojaza fomu za mali na madeni za viongozi wa umma.