URAIA: Mrundi wa UVCCM jela

Dar es Salaam. Katibu wa Umoja wa Vijana CCM kata ya Hananasifu, Mohamed Nyandu amehukumiwa kulipa faini ya Sh1.5 milioni au kwenda jela miaka mitatu baada ya kukutwa na hatia ya kuishi nchini bila kibali akijua ni raia wa Burundi.

Hata hivyo, mshtakiwa alishindwa kulipa faini na atatumikia kifungo cha miaka mitatu gerezani.

Hatua hiyo inatokana na mahakama hiyo kumtia hatiani Nyandu baada ya kukiri makosa ya kuingia, kuishi nchini kinyume na sheria ya uhamiaji na kutoa taarifa za uongo zikihusisha uraia wake.

Hukumu hiyo ilisomwa jana na hakimu Vicky Mwaikambo baada ya mshtakiwa kukiri mashtaka matatu.

Vicky alisema kutokana na mshtakiwa kukiri mashtaka yanayomkabili, Mahakama imemtia hatiani na kumtaka kulipa faini ya Sh500,000 kila kosa au kwenda jela miaka mitatu na akitoka arudishwe nchini Burundi.

Akisomewa hati ya mashtaka na wakili wa Uhamiaji, Godfrey Ngwijo alidai tarehe, mwezi na mwaka usiojulikana mshtakiwa aliingia nchini kwa kutumia njia zisizo halali na alikamatwa Januari 20 na maofisa wa uhamiaji wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Ngwijo alidai Januari 20 katika ofisi za uhamiaji wilaya ya Kinondoni mshtakiwa alikamatwa kwa kosa la kuishi nchini isivyo halali, ilhali akijua ni raia wa Burundi.

Katika shtaka la tatu mshtakiwa alitoa taarifa za uongo zikihusisha uraia wake kwa maofisa uhamiaji ili kujipatia kitambulisho cha taifa, wakati akijua siyo raia.

Ngwijo alidai hawana rekodi ya makosa ya nyuma hivyo mshtakiwa anavyoonekana amejihusisha na siasa muda mrefu, hivyo hawajui lengo lake ukizingatia hali kisiasa wa nchi aliyotoka mambo ya usalama hayapo vizuri.

“Naiomba Mahakama hii impe adhabu kali kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo,” alidai.

Baada ya hakimu Vicky kumhukumu kulipa faini ya Sh1.5 milioni, mshtakiwa alishindwa na kupelekwa gerezani kutumikia kifungo.