Msafara kamati ya ulinzi na usalama Kyela washambuliwa kwa mawe

Thursday August 29 2019

By Hawa Mathias, Mwananchi [email protected]

Kyela. Msafara wa wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Kyela umezuiwa na kundi la vijana waliovalia mashati mekundu.

Vijana hao walipanga mawe na magogo barabarani na kusababisha magari ya viongozi wa kamati hiyo kusimama. Miongoni mwa waliokuwepo katika msafara huo ni mkuu wa Wilaya ya Kyela, Claudia Kitta.

Akizungumza leo Alhamisi 29, 2019 mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Hunter Mwakifuna amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, akibainisha kuwa ilikuwa jana Jumatano Agosti 28, 2019 saa 11 jioni katika kijiji cha Mpuguti kata ya Makwale.

Amesema walikuwa wakitoka  kukagua miradi itakayotembelewa  na mbio za mwenge wa uhuru wilayani humo Jumatatu Septemba 9, 2019.

Amebainisha kuwa katika tukio hilo watu wawili wamejeruhiwa kwa mawe  akiwepo  ofisa usalama wa wilaya hiyo na katibu wake.

“Tunashukuru Mungu vyombo vyetu vya usalama vilikuwa makini katika mapambano, gari ya mkuu wa wilaya iligeuzwa na kurudi ilipotoka,” amesema.

Advertisement

Amebainisha kuwa mpaka sasa watu 45 wanashikiliwa na polisi wakihusishwa na tukio hilo, bado uchunguzi unaendelea.

 


Advertisement