Msajili wa vyama vya siasa alivyoilima CCM barua mbili

Dar es Salaam. Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema chama hicho kimeshaandikiwa barua mbili na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutokana na utovu wa nidhamu uliofanywa na wanachama wake.

Akizungumza na wahariri wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) juzi, Dk Bashiru alisema kwa nyakati mbili tofauti msajili amemuandikia barua za kujieleza kutokana na kauli “za ajabu” za viongozi wa chama hicho.

Kauli hizo ni zile alizozitaja kuwa ni “matamshi ya ajabu” yaliyotolewa na mmoja wa viongozi wa vijana wa CCM mkoani Iringa na kitendo cha ubebaji wa jeneza uliofanywa na wanachama wao mkoani Mbeya wakiigiza kuizika Chadema.

Licha ya Dk Bashiru kutotaja moja kwa moja wahusika, tukio la Mbeya lilitokea Tukuyu wilayani Rungwe Septemba mwaka juzi wakati wa hafla ya kufunga kambi ya vijana wa CCM mbele ya Naibu Spika, Dk Tulia Ackson aliyekuwa mgeni rasmi.

Picha ya video iliyosambaa mitandaoni inamuonyesha Dk Tulia akiingia eneo lililokuwa na vilio mithili ya msiba na alikwenda kukaa mbele ya jeneza hilo.

Mkoani Iringa, Dk Bashiru alikuwa akirejea kauli ya mwenyekiti wa UVCCM wa mkoa, Kennani Kihongosi aliyesema kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe anapaswa kuuawa.

“Yuko kijana mmoja Iringa, katika mjadala kuhusu tunyimwe au tusinyimwe msaada. Karopoka maneno machafu kabisa. Maneno machafu,” alisema Dk Bashiru.

“Nimeandikiwa barua na Msajili nijieleze, nimejieleza. Nimemwita yule kijana. Mimi imebidi nianze kujieleza hata katika gazeti la Mwananchi hapa; jamani hili la huyu, sisi si watu wa kupanga kuua mtu.”

Dk Bashiru alisema hiyo inatokana na baadhi ya viongozi kuchokonoa misingi ya kitaifa kwa maslahi finyu ya kisiasa.

Kuhusu suala hilo, naibu msajili wa vyama vya siasa, Sisty Nyahoza alisema wamekuwa wakiviandikia vyama vyote wanapobaini kuna uvunjaji wa sheria na kanuni.

“Ni kweli barua hizo tuliwaandikia na wakajibu,” alisema.

“Sisi kila chama tukiona kuna uvunjaji wa kanuni au sheria tunakiandikia. Lakini vyama vingine ukiviandikia vinakwenda kuzitangaza. Wengine wanajibu bila ya kutangaza.