Msanii Kala Jeremiah atamani U - rais

Msanii wa muziki wa Hiphopo nchini Tanzania, Kala  Jeremiah.

Muktasari:

Msanii wa muziki wa Hip hop nchini Tanzania, Kala  Jeremiah, amesema endapo ataingia kwenye siasa atagombea Urais.

Msanii wa muziki wa Hiphopo nchini Tanzania, Kala  Jeremiah, amesema endapo ataingia kwenye siasa angependa kugombea nafasi ya Urais.

Kala ambaye ni zao la Bongo Star Search (BSS 2007) na balozi wa vijana, ameyasema hayo  Jumatatu Oktoba 21, 2019 katika mahojiano maalumu na Mwananchi lililotaka kujua kama ana ndoto zozote za kuingia kwenye siasa  na angependa kugombea  nafasi gani.

“Kwani naamini nikiwa rais mitazamo, maono na  fikra zangu nitazileta kivitendo kwa wananchi, kwa kuwa nitakuwa na uwezo wa kuileta Tanzania ninayo iona kichwani kwangu,” alisema.

Jeremiah amesema ni kweli muziki wake umekuwa ukifananishwa na mwanasiasa jambo ambalo pia limewasukuma watu wengi kumtaka aingie kwenye siasa, lakini kutokana na kubanwa na mambo mengi, ameona asubiri kwanza.

Akizungumzia namna anavyowaona wasanii ambao kwa sasa ni wabunge, amesema wamejitahidi kuwapigania wasanii kwa kuwa wanajua changamoto nyingi zilizopo katika tasnia hiyo ya sanaa isipokuwa wakati mwingine mazingira yaliyopo ndiyo yanakuwa changamoto kwao kwa baadhi ya mambo kutekelezwa.

Katika hatua nyingine, ametoa wito kwa vijana kujitokeza kugombea nafasi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuwachagua viongozi watakaofaa kwa kuwa kura yao ndiyo  sauti zao.