Mshirika ya umma 43 Tanzania hayana bodi ya wakurugenzi

Muktasari:

  • Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonyesha kuwa mashirika ya umma 43 nchini Tanzania hayana bodi za wakurugenzi jambo lililoelezwa kuathiri  usimamizi na utekelezaji wa shughuli zake.

Dar es Salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonyesha kuwa mashirika ya umma 43 nchini Tanzania hayana bodi za wakurugenzi jambo lililoelezwa kuathiri  usimamizi na utekelezaji wa shughuli zake.

Mashirika hayo ni Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Kituo cha Elimu Kibaha (KEC),  Taasisi ya Kansa ya Ocean Road (ORCI), Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere, Shirika la Bima la Taifa (NIC), Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).

Mengine ni Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (GBT), Tume ya Nguvu ya Atomic Tanzania (TAEC), Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB).

Pia lipo Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA CCC), Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania, Bodi ya Maziwa Tanzania na Shirika la Viwango Tanzania.

Mashirika mengine yaliyotajwa kwenye ripoti hiyo ni Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira za Tabora, Mtwara, Rukwa, Mpanda, Bukoba na  Geita.

Ripoti hiyo imesema kukosekana kwa bodi kunachelewesha utekelezaji wa baadhi ya shughuli za taasisi ikiwa ni pamoja na sera na miongozo ya shirika kutoidhinishwa.

“Ninarejea maoni yangu ya miaka iliyotangulia kwamba  mamlaka za uteuzi zifikirie kuchukua hatua mapema za kuhakikisha zinafanya utambuzi wa bodi ambazo muda wake unakaribia kuisha na hivyo kuanza mchakato wa uteuzi ili kuondoa changamoto hii,” iliandika sehemu ya ripoti hiyo.

Imeagiza  kufanya tathmini ya utendaji wa wenyeviti wa bodi na wakurugenzi wanaokaimu na kufikiria kupunguza idadi ya wanaokaimu na kufanya uteuzi kamili.