Mshtakiwa wa nne kesi ya Gugai wa Takukuru akiri kosa

Muktasari:

Yasini Katera, amehukumiwa kulipa faini ya Sh100 milioni au kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kukiri kosa katika shtaka la 40 la utakatishaji fedha kwenye kesi ya kumiliki mali  zaidi ya Sh3.6 bilioni kinyume na kipato halali inayomkabili aliyekuwa mhasibu Mkuu wa Takukuru, Godfrey Gugai.

Dar es Salaam. Yasini Katera, amehukumiwa kulipa faini ya Sh100 milioni au kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kukiri kosa katika shtaka la 40 la utakatishaji fedha kwenye kesi ya kumiliki mali  zaidi ya Sh3.6 bilioni kinyume na kipato halali inayomkabili aliyekuwa mhasibu Mkuu wa Takukuru, Godfrey Gugai.

Hukumu hiyo imetolewa leo Ijumaa Oktoba 4, 2019 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya hakimu mkuu Thomas Simba. Mahakama hiyo pia imetaifisha nyumba yake iliyopo kwenye kiwanja kitalu namba 438 na 439.

Hakimu Simba amesema katika shtaka hilo, Katera atalipa faini ya sh100 milioni akishindwa kulipa fedha hizo atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela.

Amesema ametoa adhabu hiyo baada ya kuona mshtakiwa huyo amekaa mahabusu zaidi ya miaka miwili, afya yake sio nzuri na hajaisumbua mahakama na ni mkosaji wa mara ya kwanza.

"Hivyo mahakama hii inakupa adhabu ya kulipa faini ya Sh100 milioni na nyumba iliyopo kwenye  kitalu namba 438 na 439 inataifishwa inarudi serikalini na akishindwa kulipa utaenda jela miaka mitatu jela," amesema Simba.

Kabla ya kupewa adhabu hiyo, upande wa mashtaka ukiwakilishwa na wakili wa serikali mkuu,  Pendo Makondo na wakili wa Serikali  mwandamizi, Awamu Mbagwa umedai kuwa Serikali haina sababu ya kumpa adhabu kubwa hivyo wanaiachia mahakama hiyo na hawana kumbukumbu yeyote kwa mshtakiwa huyo.

Mshtakiwa huyo  inadaiwa kuwa kati ya Januari 2016  jijini Mwanza alificha umiliki halali wa viwanja viwili vilivyopo Nyegezi Mwanza huku akijua ni mazalio ya jinai ya kumiliki mali isiyoelezeka.

Awali Mbagwa aliwasomea mashtaka 39 mshtakiwa Gugai, George Makaranga na Leonard Aloys na kati ya hayo 20 ni ya utakatishaji fedha na 19 ya kughushi na kukanwa na washtakiwa hao.

"Awali walikuwa wanakabiliwa na mashtaka 43 kati ya hayo  matatu tumeyaondoa ambayo  mawili ya kughushi na moja la kutakatisha fedha,” amedai Mbagwa.

Hakimu Simba ameahirisha shauri hilo hadi Oktoba 9, 2019 itakapokuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.