Msigwa ataka mpango wa kukabiliana na athari za kiuchumi kwa sababu ya corona

Muktasari:

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa ameitaka Serikali ya Tanzania  kupeleka bungeni mpango wa kukabiliana na athari za kiuchumi zitakazotokana na maambukizi ya virusi vya corona

Dodoma. Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa ameitaka Serikali ya Tanzania  kupeleka bungeni mpango wa kukabiliana na athari za kiuchumi zitakazotokana na maambukizi ya virusi vya corona.

Msigwa ametoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma leo Jumanne Machi 31, 2020 mara baada ya Spika wa Bunge,  Job Ndugai kuelezea utaratibu uliowekwa na chombo hicho cha Dola kuzuia maambukizi ya virusi hivyo kwa wabunge na wanaohudhuria mkutano wa Bunge.

Msigwa amesema wasipokuwa waangalifu na ugonjwa huo kwa kuchukua hatua za kujikinga unaweza kusababisha kifo miongoni mwao.

Amesema kwa namna anavyoliona tatizo wabunge wanaweza kujiangalia kwa kukaa kwa kupeana nafasi lakini mitaani hali ni ngumu, utekelezaji wake ni mgumu.

Amesema nchi haijaathirika na ugonjwa pekee pia kiuchumi hivyo lazima Serikali ipeleke taarifa bungeni  itakayoonyesha mipango gani ya kukabiliana na athari za kiuchumi.

“Mfano sekta ya utalii kuporomoka. Watalii hawapo, mapato hayapo Serikali ije na mpango kwa pamoja tujadiliane ni njia gani tutapita ili tujikwamue katika tatizo hili. Lakini tukienda kidogokidogo hivi haiwezi kutusaidia,” amesema mbunge huyo wa Iringa mjini.