Msimu mpya wa korosho kuzinduliwa kesho

Muktasari:

  • Vyama vikuu vya ushirika Tanecu na Mamcu vinatarajiwa kuwa vya kwanza.

Dar es Salaam. Pamoja na mabadiliko ya utaratibu, Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) imetangaza kuzinduliwa kwa minada kuanzia kesho, Alhamisi 30, 2019.

Kwenye uzinduzi huo, taarifa iliyotolewa leo na kaimu mkurugenzi mkuu wa bodi hiyo, Francis Alfred inasema minada ya kwanza itafanywa na Chama Kikuu cha Ushirika Tandahimba na Newala (Tanecu) pamoja na kile cha Masasi na Mtwara (Mamcu).

“Wakulima, wanunuzi na wadau wote wa korosho tunawahakikishia minada hii itaendeshwa kwa uwazi na ni wafanyabiashara wenye leseni pekee wataruhusiwa kushiriki,” inasomeka sehemu ya taarifa ya bodi hiyo.

Zabuni zote za ununuzi wa korosho, taarifa hiyo inasema zitafunguliwa mbele ya wakulima watakaohudhuria na wanunuzi watatakiwa kulipa kiasi chote kinachohitajika ndani ya siku nne huku vyama vidogo vya ushirika (Amcos) ziwalipe wakulima ndani ya siku 10 baada ya kufanyika mnada husika.

Baada ya mnada wa Tanecu utakaofanyika katika Amcos ya Lumana huko Newala na ule wa Mamcu utakaokuwa chini ya Amcos ya Chiungutwa katika barabara kuu ya Masasi kwenda Newala, itafutiwa na itakayofanywa na Amcos ya Madangwa hapo Novemba 2, katika Kijiji cha Chiuta.

Baada ya hapo, Chama cha Ushirika Ruangwa, Nachingwea na Liwale (Runali) kitafuata katika awamu ya nne ya minada ya msimu huu mpya na utafanya Jumapili ya Novemba 3 Ruangwa mjini. CBT imesema ratiba ya minada itakayofuata itatangazwa kupitia tovuti yake.

Alipokuwa kwenye ziara mikoa ya kusini, Rais John Magufuli aliagiza kubadilishwa kwa utaratibu wa kuomba zabuni za ununuzi wa korosho msimu huu mpya. Awali, ilipangwa kila mnunuzi apeleke maombi yake kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa au mkuu wa wilaya.

Kwenye taarifa yake, Alfred amesema maombi hayo yatakusanywa kwenye maboksi yatakayokuwapo kwenye minada husika.

Katibu wa Amcos ya Tandshimba, Juma Namang'anyula amesema wakulima wanatarajia bei ya kilo moja itakuwa zaidi ya Sh3,000 msimu huu.

“Wanunuzi wajipande kutoa bei nzuri na walipe kwa wakati kuwawezesha wakulima kufanikisha mipango yao ikiwamo kujiandaa kwa msimu ujao wa kilimo,” amesema aNamang'anyula alipozungumza na gazeti hili.

Pamoja na hayo, amesema mavuno ya mwaka huu huenda yakapungua kutokana na kutopatikana ka pembejeo za kilimo kwa wakati pamoja na mabafiliko ya tabianchi.