Mtalii wa Marekani afa maji Tanzania akimchumbia mpenzi chini ya bahari

Sunday September 22 2019

 

Pemba. Mtalii mmoja amekufa maji wakati akimchumbia mpenzi wake chini ya Bahari ya Hindi nchini Tanzania.

Kulingana na mtandao wa Sky News, Steven Weber na Kenesha Antoine walikuwa wakiishi katika hoteli moja ya mbao ambayo ipo chini ili kuwawezesha kuona kilichopo majini.

CNN ilisema Steven Weber na Kenesha Antoine walikuwa katika Kisiwa cha Pemba, nje kidogo ya pwani ya Afrika Mashariki.

Picha zilizosambaa mitandaoni zimeonyesha Weber mwenyeji wa Baton Rounge mjini Luoisiana, Marekani, alivyoogelea hadi katika dirisha moja la kioo lililopo chini ya maji akiwa na karatasi yenye ujumbe wa kumwomba Antoine kufunga naye ndoa.

Karatasi hiyo ilisomeka: “Siwezi kuzuia pumzi zangu kwa muda mrefu ili kukwambia kila kitu ninachokipenda kwako, lakini kila kitu ninachokupendea kwako nakupendea zaidi kila siku.”

Weber baadaye aliibadilisha karatasi hiyo ili kuonyesha maneno aliyokuwa ameandika upande mwingine yaliyosema: “Je, tafadhali unaweza kuwa mke wangu? Utafunga ndoa nami?”

Advertisement

Kulingana na mtandao wa Sky News, baadaye alitoa pete ya uchumba kutoka katika mfuko wake, kabla ya kuogelea na kuondoka eneo hilo.

Antoine naye alichapisha picha za kisa hicho katika facebook ambapo anaonekana akifurahia na kuweka tamko lake: Ndio! Ndio! Ndio!.

Lakini mrembo huyo baadaye alichapisha habari mbaya kwamba mpenzi wake alifariki.

Antoine alisema kwamba hakurudi akiwa mzima baada ya kuogelea baharini.

Antoine aliandika: “Hakuna maneno yatakayotoa heshima kwa mpenzi wangu Steven Weber Jr.

“Hukutokea tena kutoka kina hicho cha bahari, hivyo basi hukuweza kusikia nikikubali mara milioni kwamba ndio nitafunga ndoa nawe!

“Hakutuweza kukumbatiana na kusherehekea mwanzo wa maisha yetu yaliyosalia, baada ya siku bora zaidi katika maisha yetu kuwa mbaya zaidi.

“Nitajaribu kujifariji kwa kuwa tulifurahia siku zetu za hivi karibuni na sote tulikuwa tumejawa na furaha wakati wetu wa mwisho”.

Wizara ya mambo ya Nje ya Marekani imesema mtalii mmoja wa Marekani amefariki nchini Tanzania lakini hakuna maelezo zaidi yaliyoripotiwa.

“Tunatoa salamu zetu za rambirambi kwa familia kufuatia tukio hili. Tuko tayari kutoa ushirikiano wowote unaohitajika,” ilisema wizara hiyo.

Kwa mujibu wa CNN, Manta Resort, hoteli waliyokuwa wapenzi hao ilitoa taarifa  Jumamosi ikithibitisha kifo hicho.

“Salamu zetu za rambirambi  na sala zinaelekezwa kwa mpenzi wake, familia zao na marafiki walioguswa na ajali hiyo,”  alisema Matthew Saus, Mtendani mkuu wa Manta Resort.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mamlaka za hapa nchini zinaendelea kuchunguza ajali hiyo.

Advertisement